Home Habari za michezo EDO KUMWEMBE – KITUO KINACHOFUATA KWA SIMBA NI KWA WAKUBWA WENZAO…TUTAONA UKUBWA...

EDO KUMWEMBE – KITUO KINACHOFUATA KWA SIMBA NI KWA WAKUBWA WENZAO…TUTAONA UKUBWA WAO..


KITUO Kinachofuata? Ni robo fainali. Ndicho ambacho Simba wamefanya juzi usiku baada ya kuichapa Gendamarie kwa jumla ya mabao 4-0 katika Uwanja wa Mkapa. Inatosha kusema kwamba ilikuwa mechi ya Simba.

Kila mchezaji alikuwa moto, hasa Bernard Morrison ambaye anaonekana kuchagua mechi za kufanya vizuri. Akiona mechi ni muhimu zaidi basi anapandisha kiwango chake zaidi. Ukweli ni kwamba alikuwa hashikiki.

Hakuna muda zaidi wa kuijadili Simba iliyocheza juzi. Itakuwa ni stori inayojirudiarudia. Tunachoweza kujadili zaidi ni namna gani Simba imestahili kufuzu katika kundi hili. Walikuwa na kila sababu na hawakuwaangusha Watanzania.

Sababu ya kwanza ni ukweli kwamba kama ukitoka katika michuano ya Ligi ya mabingwa wa Afrika na kisha kuangukia michuano ya Shirikisho ni lazima uonyeshe ukubwa wako. Hauwezi kutoka katika michuano ile halafu ukaangukia katika Shirikisho na bado ukaishia katika makundi.

Barani Ulaya kuna timu ambazo zinatoka katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na zinajikuta zimeangukia katika michuano ya Europa. Wale wakubwa lazima watambe. Wanaonyesha misuli yao na wanaonyesha kwamba wameangukia katika Europa kwa bahati mbaya tu.

Hiki ndicho ambacho hata CAF walikitarajia kwa Simba. Ndicho ambacho hata mashabiki wa timu nyingine walikitarajia kutoka kwa Simba. Bahati nzuri ndicho ambacho Simba walikifanya. Tofauti kubwa zaidi kwa Simba ni pale walipopata sare ugenini. Ule ni ukubwa katika soka letu Afrika. Ni pointi iliyowatofautisha wao na ASEC Mimosas. Ni pointi iliyowalinganisha na Berkane ambao nao walitoka sare na Gendamarie ugenini.

Lingekuwa jambo la kushangaza kama Simba ingeishia katika hatua ya makundi kwa sababu hata katika michuano mikubwa zaidi ya Afrika ambayo ni Ligi ya Mabingwa wao waliwahi kuvuka hatua hii msimu uliopita. Inakuaje mnashindwa katika michuano midogo?

Hata mashabiki wa Al Ahly, Vita, Kaizer Chiefs na wengineo wangejiuliza Simba wanaweza kushindwa kufuzu katika hatua ya makundi ya michuano ya Shirikisho kwa namna wanavyoweza kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani wa Taifa.

Sababu nyingine ambayo ilisababisha Simba wapite ni ukweli kwamba inawezekana ni timu ya pili kwa kuwekeza baada ya Berkaine. Bahati nzuri wote wamepita. Sina uhakika sana katika hili lakini ni wazi kwamba timu kama Gendamarie na ASEC haziwezi kuifikia Simba katika uwekezaji ndani ya kikosi katika misimu ya karibuni.

Berkane wanajulikana kwa ubabe wao wa pesa na ndio maana waliwahi kuvamia kambi za Simba na Yanga wakachukua wachezaji muhimu katika vikosi vyao, Clatous Chama na Tuisila Kisinda. Waliwachukua kwa bei mbaya ambazo zilituacha midomo wazi.

Gendamarie sidhani kama wana ubavu wa kupimana na Simba katika masuala ya fedha. Rafiki zangu ASEC ni timu ambayo imetengenezwa kama chuo hivi kwa miaka miwili. Inapika wachezaji kwa ajili ya kuwauza kwenda kwingineko.

SOMA NA HII  LWANGA : HATUKUTAKA KINGINE ZAIDI YA USHINDI DHIDI YA AL AHLY

Muda si mrefu utasikia makinda waliowika katika kikosi chao mwaka huu wapo Ulaya wakicheza katika ligi mbalimbali. Ni kitu tofauti na Simba ambao wachezaji wao wanakuwa wamefika na wamepevuka huku wakikaribia kuhitimisha maisha yao ya soka.

Katika hili hili jaribu kuangalia ni namna gani ambavyo Simba ndio timu yenye wachezaji wengi zaidi wa kigeni katika kikosi cha kwanza. Wamorocco wana kanuni zao ambazo zinawabana wachezaji wa kigeni lakini hawa ndugu zetu wengine ni ukosefu wa kiuchumi tu ndio ambao umepelekea wajaze wachezaji wazawa.

Inawezekana Simba imetumia wachezaji zaidi ya kumi wa kigeni katika mechi zake sita za makundi huku ikiwa ni timu pekee iliyotumia wachezaji wengi zaidi wa kigeni katika kundi na ikiwezekana katika michuano yenyewe mpaka sasa.

Simba pia ilikuwa na nafasi nzuri ya kupita kwa sababu ilianzia mechi nyumbani na imemalizia mechi nyumbani. Hii ina maana kubwa katika soka la Afrika. Maana yake ilikuwa ni lazima waanze na ushindi nyumbani kwa ajili ya kupata pointi tatu muhimu na kujiimarisha kiakili.

Lakini pia kuna umuhimu mkubwa kumalizia nyumbani hasa kama pambano lenyewe litahitaji pointi tatu muhimu ambazo hazina mjadala. Kama mechi hii ingechezwa Niger maisha yangekuwa magumu zaidi kwa Simba pengine kuliko pambano ambalo Simba ilipora pointi moja wakati ule.

Hatima ya Simba ilikuwa mkononi mwao na mechi ilikuwa nyumbani kwao. Sio timu nyingi ambazo zingeweza kuizuia Simba katika mechi muhimu kama hii. wameshindwa wengi kuzuia hatima ya Simba katika mechi kama hizi.

Kuna waliowahi kufanikiwa kama Stella Abidjan, UD Songo na Jwaneng Galaxy. Hata hivyo wengi walishindwa kuizuia pindi walipohitaji matokeo yao nyumbani. Wanaweza wakashindwa katika Ligi lakini mara nyingi katika michuano ya kimataifa wanageuka kuwa wanyama wengine tofauti waliobeba ukatili mkubwa kama tulivyoona juzi.

Kwa sasa Simba kituo kinachofuata ni robo fainali. Waendeleze palepale walipoishia kwamba timu ambayo inashushwa kutoka Ligi ya Mabingwa kwenda Shirikisho inapaswa kuishia mbali. Bahati mbaya kwao ni kwamba huku watakutana na wenzao.

Huku watakutana na timu kali zaidi. Kuna zile ambazo zilitolewa katika michuano ya Ligi ya Mabingwa kisha wakashushwa chini kucheza Shirikisho. Na kuna wale ambao walianzia chini katika michuano hii hii lakini wanajulikana kwa ukali wao.

Hapa kidogo kutakuwa na kipimo kwa yeyote ambaye atapangwa na Simba. Itakuwa tofauti kidogo na mechi kama hizi za kina Gendamarie. Hata hivyo hauwezi kufika fainali za michuano ya Afrika au kuchukua mataji kwa kupangiwa na timu ndogo. Lazima utakutana na wakubwa wenzako.

Makala haya yaliandikwa na Edo Kumwembe na kuchapishwa kwanza kwenye wavuti la MwanaSpoti.