SIKU ya sikukuu ya Pasaka Aprili 17, Simba watakuwa Dar es Salaam wakikiwasha na Orlando Pirates kwenye mechi ya kwanza ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho lakini wakaonyeshwa mitego kadhaa.
Orlando wana safu kali ya ushambuliaji kwani kwenye michezo 10 iliyopita ya mashindano yote, wamefunga mabao 18.
Hiyo inamaana kuwa wana wastani unaokaribia mabao mawili kufunga kwenye kila mchezo, dakika ambazo wanaonekana kuwa ni hatari zaidi ni zile za kipindi cha pili kwani kwenye idadi hiyo ya mabao wamefunga 10 wamefunga hapo.
Lakini wanafungika kwani ndani ya michezo 10 iliyopita, wameruhusu nyavu zao kuguswa mara 10,wanawastani wa kufungwa bao moja kwenye kila mchezo. Takwimu zao zinaonyesha kuwa kati ya mabao 10 waliyofungwa manane yalikuwa kipindi cha kwanza na wachambuzi wametafsiri kwamba ndio muda wa Simba kuutumia.
Kwenye michezo 10 iliyopita kwa Orlando Pirates, wameshinda minne, mitatu ikiwa ya kombe la Shirikisho ambapo ni dhidi ya Soura (2-0) na Royal Leopards mara mbili (3-0, 6-2) na mmoja ukiwa wa Ligi Kuu Afrika Kusini dhidi ya SuperSport United(3-2). Wametoka suluhu tatu ambapo moja ni ya Shirikisho dhidi ya Al-Ittihad (0-0) ,nyingine zikiwa kwenye ligi dhidi ya Golden Arrows na Cape Town City. Wamepoteza michezo mitatu ambayo ni dhidi ya Marumo Gallants kwenye kombe la ligi kwa mikwaju ya penalti 5-4, Kaizer Chief (2-1) na Al-Ittihad kwenye mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi (3-2).
Mshambuliaji wa zamani Simba, Bakari Kigodeko alisema; “Simba wanatakiwa kucheza kwa nidhamu kwa sababu bila nidhamu hawatoweza kufika popote na wachezaji muhimu wajitambue.”
Mwaka jana Simba walitolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kaizer Chiefs walikuwa wanashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi, Orlando nao kwasasa wanashika nafasi ya tano.
Lakini Orlando safu yao ya ushambuliaji wanaye Bandile Shandu ambaye kwenye mechi sita za Shirikisho amefunga mabao manne.
Orlando wanaonekana kuwa na nidhamu ya kutosha wanapokuwa uwanjani baada kucheza mechi sita za makundi na kupata kadi za njano sita na nyekundu moja huku Simba wao wakipata kadi za njano 16. Mafanikio ya Simba tayari yameipa Tanzania timu 4 za kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao. Mnyama anataka kucheza fainali msimu huu.