BAADA ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kutangaza michezo yote ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kuamuliwa na teknolojia ya Video Assistants Referee (VAR) kwa Tanzania itahusisha taasisi nne.
Ikiwa ni kwa mara ya kwanza kwa VAR kutumika Tanzania itatumika Uwanja wa Benjamin Mkapa kwenye mechi ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho kati ya wenyeji Simba na Orlando Pirates kutoka Afrika ya Kusini.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Ofisa habari wa Simba Ahmed Ally ameeleza kuwa historia hiyo ya kutumia VAR kwa mara ya kwanza Tanzania itawekwa kwa usimamizi wa taasisi nne ambazo ni CAF, TFF, Azam TV na Simba.
“Azam tunafanya nao kazi kwa karibu pia ndio wenye haki za matangazo kwa hapa nchini hivyo tutaungana nao sambamba na CAF, TFF kuhakikisha kila kitu kinaenda ipaswavyo,” alisema Ahmed na kuongeza;
Tayari taasisi hizo zimefanya vikao na zinaendelea na vikao vikubwa vikubwa ili kuhakikisha hakiharibiki kitu na naamini itakuwa hivyo.”
Aidha Ahmed ameweka wazi kuwa bado hawajapata taarifa rasmi, mpinzani wao Pirates anakuja lini nchini lakini kuanzia leo watajulishwa na watatangaza taratibu zinazofuata.
Pia ameendelea kueleza kuwa waamuzi watakaochezesha mwchi hiyo watawasili Tanzania April 14 huku wale wasimamizi wa VAR wakitarajiwa kufika April 15.
Simba itajitupa Uwanja wa Mkapa April 17 kucheza na Pirates mechi ya kwanza ya robo fainali na mechi ya marudiano itapigwa April 24 na mshindi wa jumla atatinga nusu fainali ya michuano hiyo.