Home Habari za michezo KISA ‘MASHUSHU’ WA WASAUZI…..SIMBA KUIKIMBIA KAMBI YAO YA MBWENI…WATAKA MATOKEO KAMA YA...

KISA ‘MASHUSHU’ WA WASAUZI…..SIMBA KUIKIMBIA KAMBI YAO YA MBWENI…WATAKA MATOKEO KAMA YA ASEC…


KATIKA kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wa kwanza nyumbani dhidi ya Orlando Pirates, uongozi wa Simba umepanga kuwahamisha kambi wachezaji wa kikosi hicho akiwemo Bernard Morrison na Pape Ousmane Sakho na kuwaficha sehemu tulivu zaidi.

Uamuzi huo umekuja baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Pablo Franco kuomba sehemu yenye utulivu na ulinzi maradufu utakaowafanya wachezaji wake akili zao kuwaza mechi hiyo pekee.

Mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika unaotarajiwa kuchezwa Jumapili ya wiki hii kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar, Simba inahitaji ushindi mzuri kabla ya kurudiana Aprili 24, nchini Afrika Kusini kuona hatma yao ya kwenda nusu fainali.

Katika mchezo huo, Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limewaruhusu Simba kuingiza mashabiki 60,000, pia kutakuwa na teknolojia ya VAR, ikiwa ni mara ya kwanza kutokea Tanzania.

Chanzo makini kutoka Simba, kimeliambia Spoti Xtra kwamba: “Kocha aliomba kupatiwa sehemu tulivu na yenye ulinzi mkali ambayo itawafanya wachezaji wake kuwa na utulivu kipindi hiki cha kujiandaa na mchezo muhimu dhidi ya Orlando Pirates.

“Uongozi umemkubalia na kupanga kuhamisha kambi siku chache kabla ya mechi kutoka Mbweni na kuweka mjini kama ambavyo walifanya wakati tunajiandaa na mchezo wa kwanza wa makundi msimu huu dhidi ya ASEC Mimosas tuliocheza hapa nyumbani na kushinda 3-1.

“Unajua hii ni sehemu ya mbinu ambayo tunaitumia kuhakikisha tunaziba mianya yote ya wale ambao hawatutakii mema kuzikwepa hujuma zao. Lengo letu ni kushinda na kwenda nusu fainali.”

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, alisema: “Kuna uwezekano wa kuhamisha kambi kutoka pale kwa siku zote, hii ni kwa ajili ya ulinzi zaidi.”

Hii ni mara ya pili msimu huu katika michuano hiyo Simba inafanya tukio kama hilo ambapo walipokuwa wakijiandaa na mchezo wa kwanza wa makundi dhidi ya ASEC Mimosas uliochezwa Februari 13, Uwanja wa Mkapa, walihama kambi na kujificha katika Hoteli ya Element by Westin Dar es Salaam, iliyopo Masaki.

SOMA NA HII  TUISILA KISINDA AFUNGUKIA ISHU YAKE YA KUIBUKIA NDANI YA SIMBA