KIUNGO Mshambuliaji wa Yanga, Chico Ushindi, tangu ajiunge na timu hiyo amekuwa akikumbwa na majeraha ya mara kwa mara hali inayomfanya kushindwa kuonesha ubora ambao Wanayanga wana uhitaji.
Nyota huyo aliyejiunga na Yanga katika usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea TP Mazembe, majeraha makubwa yanayomsumbua ni kupata maumivu ya nyama za paja.
Hivi karibuni, nyota huyo kutoka DR Congo, aliukosa mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam Sports dhidi ya Geita Gold baada ya kupata majeraha hayo.
Chanzo chetu kutoka Avic Town, Kigamboni, Dar, ilipo Kambi ya Yanga, kimesema kuwa: “Chico alipata majeraha ya nyama za paja akiwa mazoezini wakati kikosi kikijiandaa na mchezo wa michuano ya Shirikisho dhidi ya Geita Gold.
“Unajua hayo majeraha yanaweza kukupata wakati wowote, lakini kwa sasa yupo fiti na ataanza mazoezi na timu, huenda akacheza mechi inayofuata dhidi ya Simba.”
Akizungumza, Daktari wa Yanga, Sheik Mngazija alisema: “Kuhusu suala la majeraha ya Ushindi (Chico) kwa sasa amepona na ataanza mazoezi na timu tutakapoanza maandalizi ya mchezo ujao.”
Katika mechi za kimashindano alizocheza, Chico Ushindi bado hajafunga bao.