Home Habari za michezo HII NDIVYO WASAUZI WALIVYOIPA SIMBA RAMANI YA VITA BUREEEE..MCHEZO UJAO NI ‘KUMSUKUMA...

HII NDIVYO WASAUZI WALIVYOIPA SIMBA RAMANI YA VITA BUREEEE..MCHEZO UJAO NI ‘KUMSUKUMA MLEVI TU’…


Ushindi wa bao 1-0 ambao Simba imeupata dhidi ya Orlando Pirates unaweza usiwe jambo kubwa kwao lakini darasa walilolipata linaweza kuwa silaha muhimu kuelekea mechi ya marudiano ugenini, Jumapili ijayo, Aprili 24.

Uimara na udhaifu ulioonyeshwa na Simba katika baadhi ya maeneo kwenye mchezo huo wa juzi unaweza kuwa fursa nzuri kwa benchi la ufundi kuvifanyia kazi ili iweze kupata matokeo mazuri katika mechi ya marudiano ili iweze kusonga mbele na kutinga hatua ya nusu fainali.

Nidhamu ya ulinzi ambayo wachezaji wa Simba walionyesha pindi walipokuwa wanashambuliwa na Orlando Pirates ni jambo ambalo wawakilishi hao wa Tanzania wanapaswa kuliimarisha zaidi katika mechi ya marudiano ambayo wanahitaji matokeo ya ushindi au sare ya aina yoyote ili waandike historia ya kucheza nusu fainali ya mashindano hayo kwa mara ya kwanza.

Lakini, udhaifu wa safu ya kiungo hasa kuisogeza timu mbele pale walipounasa mpira kutoka kwa wapinzani na uharaka wa kufanya uamuzi kwa wachezaji wake hasa katika kushambulia pia vinapaswa kufanyiwa kazi ndani ya kipindi cha wiki moja iliyobaki kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa katika Uwanja wa Orlando jijini Johannesburg.

KASI NDOGO MCHEZONI ILIICHELEWESHA SIMBA

Simba walianza mchezo kwa kasi ya chini jambo ambalo lilikuwa na faida kwa wageni, Orlando Pirates kutimiza mpango wao wa kutoruhusu mabao ya mapema.

Muda mwingi Simba ilipiga pasi za pembeni na nyuma na kusogea taratibu langoni mwa Orlando Pirates jambo lililowafanya wapinzani kujipanga kwa haraka kuziba mianya na kupelekea ugumu kwa Simba kulisogelea lango lao.

Kwa bahati mbaya Peter Banda na Bernard Morrison ambao walipokea mipira mingi pembeni mwa uwanja, walikosa ujasiri wa kuvunja ukuta waliowekewa na wapinzani wakati walipokuwa wanashambulia.

Lakini pia katikati mwa uwanja walianza na viungo wawili ambao kiasili huwa wanacheza zaidi nyuma ya mstari unaougawa uwanja, Taddeo Lwanga na Jonas Mkude jambo ambalo lilitengeneza ombwe kubwa kati yao na wachezaji wa nafasi ya ushambuliaji na hivyo kuwapa uhuru mkubwa viungo wa Orlando Pirates.

SOMA NA HII  WAPINZANI WA YANGA HALI TETE...WANA NJAA HATARI TIMU HAINA PESA...JE WATAKUJA?

Pindi alipoingia Rally Bwalya akichukua nafasi ya Taddeo, kasi ya Simba iliongezeka na angalau ilionekana kuwapa wakati mgumu viungo na walinzi wa timu pinzani.

UBORA SILAHA YA ORLANDO PIRATES

Moja ya mambo yaliyoibeba Orlando Pirates katika mchezo wa juzi ni kiwango binafsi cha mchezaji mmojammoja tofauti na Simba ambayo ilitegemea zaidi uwezo wa kitimu.

Pindi Simba walipokuwa wanamiliki mpira, wengi walifika kwa wakati katika maeneo waliyotakiwa kuwepo kimbinu na kuziba nafasi na pindi walipounasa mpira walijua wapi pa kuupeleka na nini wakifanye kutengeneza nafasi.

Waliwalazimisha Simba kushambulia zaidi kutokea pembeni badala ya katikati na ikawa rahisi kwao kuokoa aina hiyo ya mashambulizi.

SOMO LA VAR

Inawezekana kabla ya mchezo mashabiki wengi wa soka nchini hawakuwa wakifahamu ni kwa namna gani teknolojia ya Video ya usaidizi kwa waamuzi (VAR) inafanya kazi.

Wengi waliamini kuwa ikiwepo na kunapotokea tukio lolote ambalo litalalamikiwa ni lazima mwamuzi kwenda kujiridhisha kwa kutazama upya kisha kutoa uamuzi.

Hata hivyo, kwa mujibu wa mwongozo wa VAR, sio lazima kwa refa kwenda kujiridhisha baada ya kufanya uamuzi na inaweza kuwepo na isitumiwe na mwamuzi kama alivyoonyesha mwamuzi Haythem Guirat kutoka Tunisia.

UTULIVU UTAIBEBA SIMBA

Hakuna mechi rahisi ugenini hasa unapocheza katika bara hili la Afrika.

Ni wazi kwamba Simba itakutana na presha na changamoto nyingi ugenini huko Afrika Kusini ili kuwatoa mchezoni katika mechi ya marudiano lakini kama timu itaandaliwa vyema kimbinu na kisaikolojia bado ina nafasi ya kufanya vyema na kusonga mbele.

Haipaswi kuruhusu muingiliano baina ya timu na watu wa kawaida hotelini na inapaswa kuchukua tahadhali ya kila hujuma ambayo itaandaliwa na wenyeji kwa lengo la kuwavuruga.

Lakini pia wachezaji wake wanapaswa kucheza kwa nidhamu kubwa katika dakika zote 90 za mchezo na pia wajiepushe na makosa ya kinidhamu ambayo yanaweza kuwasababishia kadi na kuwapa wapinzani wao faulo au penalti ambazo zinaweza kuwamaliza. Kila la heri Simba katika mechi ya marudiano itakayopigwa Sauzi.