Home Habari za michezo BAADA YA ORLANDO KUANZA FIGISU FIGISU DHIDI YA SIMBA…UBALOZI WA TZ AFRIKA...

BAADA YA ORLANDO KUANZA FIGISU FIGISU DHIDI YA SIMBA…UBALOZI WA TZ AFRIKA KUSINI WATOA TAMKO HILI….


Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Meja Jenerali Mstaafu, Gaudence Milanzi amewahakikishia Wachezaji, Benchi la Ufundi na baadhi ya Viongozi wa Simba SC ulinzi mkali wakati wote watakapokua nchini humo.

Kikosi cha Simba SC juzi Ijumaa (April 22) kiliwasili mjini Johannesburg-Afrika Kusini kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, utakaochezwa leo Jumapili (April 24).

Balozi Milanzi amewataka wachezaji wa Simba SC kuhamishia akili zao uwanjani kwa ajili ya kupata ushindi na kamwe wasiwaze kitu chochote cha nje ya jukumu linalowakabili.

Milanzi amesema maofisa wake wamejipanga imara kuhakikisha mambo yote yanakwenda vyema na wachezaji wafikirie mchezo huo wa marudiano tu.

“Tulikuwa na kikao wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Afrika Kusini kuhusu masuala mbalimbali, tukagusia pia na suala la michezo, kwa sababu ni sehemu ya kuweka ushirikiano, tuliligusia, unajua Simba inajulikana kila sehemu, hata huku inazungumzwa sana, tukaona tunaweza kufanya haya yanayotokea yasiwe kama wanavyozungumzwa.”

“Tunaamini ni maneno ya kishabiki, nawaomba wachezaji wa Simba wayaache, wao wajikite zaidi uwanjani, akili yao iwe kucheza mpira kwa ajili ya kutafuta ushindi, kwa suala la ulinzi Serikali ya Afrika Kusini haina matatizo,” amesema balozi huyo

Kauli hii ya kuhakikishiwa ulinzi imekuja baada ya kocha wa Orlando Pirates, Mandla Ncikazi, kuzungumza maneno makali, ambayo yameonekana kuwatisha Simba SC, hivyo kuhitaji ulinzi.

Mbali na hilo, Milanzi ameipongeza Simba SC kwa ushindi waliopata katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza wakiwa nyumbani na kusema walicheza vizuri kwa kumiliki mpira kwa kiasi kikubwa, hivyo anaamini wataendelea kufanya vyema.

“Niwapongeze Simba SC kama kawaida yao, kwa mara nyingine tena wameiwakilisha nchi vizuri, walicheza vizuri sana, na nawaomba katika mechi hii ya marudiano wacheze kama vile, wasicheze kwa kuzuia sana, washambulie pia kwa ajili ya kupata ushindi,” amesema Balozi Milanzi.

Katika mchezo huo Orlando Pirates itapaswa kusaka ushindi wa mabao mawili ama zaidi ili kujihakikishai nafasi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika, huku Simba SC ikipaswa kupambana kusaka ushindi wowote ama kulinda ushindi walioupata Dar es salaam wa bao 1-0.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA MBELE GAZETI LA SPOTI XTRA ALHAMISI