Home Habari za michezo MPOLE AZIDI ‘KUKIMBIZA MWIZI KIMYA KIMYA’….MAYELE AJIPANGE LA SIVYO ANAACHWA MAZIMA…

MPOLE AZIDI ‘KUKIMBIZA MWIZI KIMYA KIMYA’….MAYELE AJIPANGE LA SIVYO ANAACHWA MAZIMA…


MSHAMBULIAJI hatari wa Geita Gold, George Mpole amezidi kuonyesha makali yake ya kutupia kwenye Ligi Kuu baada ya kuendelea kumfukuzia nyota wa Yanga, Fiston Mayele.

Mpole amefunga bao moja leo kwenye ushindi wa timu yake ya Geita Gold wa mabao 2-0 dhidi ya KMC kwenye uwanja wa Nyankumbu mjini Geita.

Bao hilo ni la 10 kwa Mpole msimu huu katika ligi akiwa pungufu ya bao moja dhidi ya Mayele ambaye anaongoza orodha ya wafungaji akiwa amepachika kambani mabao 12.

Katika mchezo huo wa ligi uliopigwa saa 10 jioni huku ukiambatana na mvua Geita Gold imetumia vyema uwanja wa nyumbani ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Mchezo huo ulikuwa mgumu kwa pande zote na kumaliza dakika 45 bila mbabe lakini Geita Gold warejea kipindi cha pili wakiwa bora zaidi na kupata mabao hayo mawili ambayo yamepachikwa na mlinzi Amosi Kadikilo dakika ya 47 na George Mpole dakika ya 75.

Ushindi huo wa pili mfululizo kwenye ligi umeipandisha Geita Gold kwenye msimamo kutoka nafasi ya tisa hadi ya tano ikifikisha pointi 27 huku KMC ikishuka kwa nafasi moja hadi ya tisa na alama zao 24.

Kuingia kwenye nafasi tano za juu katika ligi kwa mara ya kwanza kwa Geita Gold ni sehemu ya mipango yao tangu mwanzo wa msimu ambapo klabu hiyo imejizatiti kuhakikisha inamaliza kwenye nafasi hizo tano.

SOMA NA HII  KOCHA SINGIDA BS AITELEKEZA TIMU...KUTIMKIA MAREKANI...ISHU NZIMA IKO HIVI A-Z