Home Habari za michezo MAN UTD KUMCHUKUA ERIK TEN HAG NI SAWA NA KUKUBALI KUWEKA...

MAN UTD KUMCHUKUA ERIK TEN HAG NI SAWA NA KUKUBALI KUWEKA BUNDUKI CHINI..MIKONI JUU…


Saddam Hussein alipuuza kila amri ya Wamarekani walipotaka ajisalimishe. Akakubali waje. Hakutaka kuondoka katika ardhi yake. Hakutaka kuondoka alipo.

Alihisi bado ana nguvu ya kupambana. Mwisho alikutwa katika shimo la ovyo kando ya mtaro. “Mimi ni Saddam Hussein Rais wa Iraq. Tunaweza kuongea?” Saddam aliwaambia wanajeshi wa Marekani. Alikuwa amechelewa. Kilichobaki ni historia. Sio hadithi inayosisimua sana, lakini kuna wakati inabidi upime nguvu zako na usijidanganye. Kwa kifupi usijidanganye kama ambavyo Manchester United walijaribu kujidanganya kwa miaka sasa.

Nguvu yao ilikuwa imekwisha. Hata hivyo bado walikuwa wanaamini kwamba wana nguvu. Manchester City na Liverpool wametawala soka la Kiingereza kwa sasa wakifuatiwa na Chelsea, lakini United walikuwa wanajiona kama vile bado wamo. Kama vile walikuwa wakifanya makosa madogomadogo tu na kwamba mambo yangekaa sawa muda wowote na kuendelea pale ambapo Sir Alex Ferguson aliishia. Haikuwezekana.

United walijaribu kuleta makocha wenye majina makubwa kama vile Jose Mourinho na Louis van Gaal, bado mambo hayakuwezekana. Walimleta Ole Gunnar Solskjaer ili afanye mambo ambayo Sir Alex alikuwa anafanya. Haikuwezekana. Walidhani alikuwa mtu ambaye alikuwa anaifahamu klabu na angeirudisha ilipotoka. Haikuwezekana.

Sasa hivi United wameamua kunyanyua mikono juu. Wamesalimu amri. Wamekwenda kwa kocha wa Ajax, Erik Ten Hag. Sikiliza. Sio kocha mkubwa. Wala hakuwahi kuwa mchezaji mkubwa. Lakini United wamerudi chumbani wamejifungia na kutaka kutengeneza mradi wao mpya. Unaweza kuchukua miaka kadhaa lakini wanataka kujipanga upya. Wamenyoosha mikono juu.

Jurgen Klopp alipofika Liverpool alianza upya. Ukionyeshwa kikosi chake cha kwanza wakati anafika na leo Liverpool inavyopangwa utajua alianza upya. Wakati huo alikuwa na kina Martin Skirtel leo na kina Virgil Van Dijik. Sitaki kutaja maeneo mengine lakini ameisafisha Liverpool na kuiweka katika mfumo anaoutaka yeye. Kwa kila kitu. Pep Guardiola alipofika Manchester City alianza mradi wake upya. Sawa kuna kina Roberto Mancini ambao walishashinda vitu kabla yake, lakini yeye akaamua kuutengeneza mpira wake ambao leo unaendelea kutusumbua. Akaondoa kina Nicolas Ortamendi, Joe Hart, Pablo Zabaleta, Yaya Toure na wengineo. Akaweka mpira wake.

Arsenal ndio ambao nao walinyoosha mikono pia. Waliposuasua baada ya Arsene Wenger kuondoka wakahisi wanaweza kuendelea walipoishia. Wakamchukua Unai Emery. Aliposuasua wakamchukua kocha ambaye hakuwahi kuwa kocha mkuu hapo awali, Mikel Arteta. Msaidizi wa Pep Guardiola.

Arsenal waliamua kumkabidhi timu Arteta aanze upya. Na kweli Arteta ameanza upya. Alianza fagio lake taratibu kwa kina Saed Kolasinac, Nacho Monreal, Mesut Ozil, Hector Bellerin na sasa Pierre-Emerick Aubameyang. Akaanza kuwaamini watu wake ambao wengi ni vijana. Imemchukua muda lakini sasa Arsenal inaeleweka. Nani alijua kwamba leo April wangekuwa wanagombania kuingia Top Four licha ya kuondoka kwa kina Ozil na Auba? Sawa wametoka kufungwa mechi tatu mfululizo, lakini bado wapo katika mwendo na bado wana asilimia nyingi za kwenda Top Four. Msimu ujao wataimarika zaidi wakichukua wachezaji ambao wanawataka.

Lakini inatosha kusema wamempa timu Arteta awatengezee wakiamini ana falsafa za makocha wa kisasa, na pia ana falsafa za mpira wa kisasa. Kwa msimu huu unaweza kuona Arsenal wameanza kupata mwelekeo kuliko United. Lakini sasa United wameamua kumchagua Ten Hag. Sababu ni rahisi tu. Wameitazama Ajax inavyocheza na wanataka afanye kitu kilekile katika uwanja wa mazoezi wa Carrington na uwanja wa mechi – Old Trafford. Na kwa vile wana pesa wanaamini kwamba Ten Hag ashindwe yeye tu. Wanaamini wamepata mtu sahihi wa soka la kisasa.

SOMA NA HII  SIMBA KUFANYA USAJILI HUU WA KUTISHA...KUSHUSHA MASHINE HII HATARI

Kwa vile ambavyo Ajax inacheza unagundua kwamba United wamepata mtu sahihi zaidi ambaye atasimika falsafa zake Trafford na kurudisha heshima ya timu. Ni suala la kusubiri na kuona namna ambavyo atasimika nguvu zake katika presha kubwa. Kuna presha kubwa Manchester United kuliko Ajax. Kuna presha ya mashabiki walio wengi duniani kote. United ni kubwa zaidi. Lakini kuna presha ya kushughulika na mastaa wakubwa klabuni na ambao wana majina makubwa huku wakilipwa mabilioni ya pesa kila wiki. Hawa watamtumikia kama wale makinda wa Ajax walivyokuwa wanamtumikia?

Tunaanza na Cristiano Ronaldo. Nitajadili hili kwa kina zaidi siku zijazo, lakini makocha wa kileo wanataka mambo mengi zaidi kwa mchezaji wa nafasi za mbele zaidi ya mabao yake. Makocha hawa kina Klopp na Guardiola wanataka mambo mengi zaidi kwa mchezaji ndio maana kina Sadio Mane na Kelvin De Bruyne wanakaba kama Javier Mascherano. Hofu yangu ni kwamba miongoni mwa mambo ambayo yatakuwa mwanzo wa mradi mpya kwa Ten Hag ni pamoja na kuachana na Ronaldo. Lakini pia kuna wengi ambao nahisi wataondoka katika Manchester United hii kupisha timu mpya ambayo Ten Hag ataiunda taratibu kama ambavyo kina Klopp na Pep walianza kuunda taratibu halafu ndani ya miaka mitatu wakawa wa moto zaidi.

Hatima ya kila mchezaji naona ipo hatarini. Mchezaji ambaye naamini hayupo hatarini ni Bruno Fernandes tu. Wengine wengi wapo hatarini akiwemo rafiki yangu, Harry Jacob Maguire. Vipi kuhusu kina Luke Shaw na Aaron Wan Bissaka? Wapo wengi. Hawataondoka ndani ya msimu mmoja, lakini watapanguswa taratibu ndani ya miaka miwili au mitatu licha ya kwamba wana mikataba ya muda mrefu. Mwishowe Ten Hag ataipata timu yake ambayo itamtumikia kwa kila hali. Huu ni upande mmoja ambao nimeutumia kumuamini kocha huyu Mdachi ambaye matajiri wa Trafford wanaamini anaweza kuwa askari wao atakayewaanzishia mwendo mpya.

Upande mwingine unaogofya kidogo. Kwamba huenda Ten Hag alikuwa na ubora mwingi akiwa na Ajax kwa sababu alikuwa katika timu ndogo Ulaya katika zama hizi. Kwamba sasa anatua England katika Ligi yenye Manchester City, Liverpool, Chelsea, Arsenal, Tottenham na wadogo wengine wa mitaa ya kati ambao wanajulikana kwa viburi vyao.

Ataweza kuhimili presha ya kufundisha Manchester United? Lakini zaidi matajiri wamejitoa kwa hali na mali kumuamini awavushe hata katika mawimbi makali? Jaribu kuangalia namna ambavyo Arteta alikaribia kufukuzwa hapo mitaa ya kati. Alipoteza mechi tatu mfululizo lakini matajiri bado walimuamini na kuimeza presha ya mashabiki. 

Hata Pep wa leo hakuwa yule wa msimu wa kwanza. Alimeza presha na mashabiki pia walimeza presha. Unakumbuka alidhalilika katika msimu wa kwanza kiasi cha kuchapwa mabao 4-1 na timu kama Everton? Leo imebaki kuwa historia tu. Ameiweka Ligi Kuu ya England katika mikono yake. Hata Klopp alikuwa na wakati mgumu katika msimu wake wa kwanza. Leo ameiweka Ligi Kuu ya England katika mkono wake. Uvumilivu huu unatakiwa kwa United. Nadhani watakuwa nao kwa sababu wamejitafakari na kuamua kuanza upya. Ni jambo muhimu katika mpira wa kisasa.

United wangetaka kujiona wakubwa zaidi wangerudi kwa kocha ambaye ana jina kubwa ili aendelee pale wanapodhani waliishia na Sir Alex Ferguson 2013. Tusubiri.

1 COMMENT

  1. For most recent news you have to pay a visit world-wide-web and on web I found this website as a
    most excellent site for latest updates.

    Feel free to visit my site … Webdesign