Home Habari za michezo OKWI AWAPA YANGA VIFAA VIWILI MATATA…ONYANGO APIGWA CHINI RASMI….

OKWI AWAPA YANGA VIFAA VIWILI MATATA…ONYANGO APIGWA CHINI RASMI….


Unachotakiwa kufahamu sasa ni kwamba huko Yanga kumekucha. Na muda si mrefu utashuhudia vyuma vikipishana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

Matajiri wa Yanga wamehamishia akili yao kwenye usajili na sasa wanasuka kikosi kipya cha msimu ujao mapema na habari mpya ni kwamba jana walikuwa nchini Rwanda wakifuata viungo wawili wa kazi ambao hata staa wa zamani wa Simba Emmanuel Okwi amewavulia kofia.

Yanga imewafuata kiungo mkabaji Nshimiyimana Ismael ‘Pitchou’ na mwingine mchezeshaji Bigirimana Obed wote wanakipiga kwenye klabu kongwe ya Kiyovu.

Ramani nzima ya Yanga katika usajili wa viungo hao inachorwa na na kocha wao msaidizi Cedrick Kaze ambaye amewashtua Yanga na tayari wako Rwanda wakiwania saini za wawili hao ambao tayari wanawindwa na klabu za Uarabuni. Kaze na jopo la Yanga watawashuhudia wachezaji hao wakikiwasha leo kwenye mechi ya ligi dhidi ya Gasogi saa 10 jioni.

“Watu wa Yanga wako hapa Kigali (Rwanda) wanamalizia mazungumzo hawa ni wachezaji bora kabisa katika ligi hii tangu walipotoka Burundi wamekuwa na kiwango cha kushtua, kama watawapata itakuwa ni usajili mkubwa kwa Yanga,” alisema mmoja wa mabosi wa Kiyovu na kuongeza kuwa ni ngumu Yanga kuwakosa kwa jinsi wanavyoonekana kujipanga licha ya kufanya siri kubwa.

Licha ya Kaze kuwahakikishia Yanga juu ya ubora wa mastaa hao, lakini hata staa wa Kiyovu, Okwi naye ameulizwa mara kadhaa na viongozi kuhusiana na uwezo wa wachezaji hao akasema ni majembe kwelikweli na wanaibeba timu.

Awali, Yanga ilikuwa na mpango wa kusajili beki wa kati ikiwa na machaguo mawili, Mubarik Yussif raia wa Ghana na Joash Onyango. Lakini habari za ndani ni kwamba juzi usiku walikubaliana kwa kauli moja kupiga chini usajili wa Onyango na hawatachukua mchezaji yeyote kutoka Simba.

Yanga kama itakamilisha usajili wa viungo hao itasitisha usajili wa beki Mghana, wakipiga hesabu ya kumhamishia Yannick Bangala katika beki ya kati, nafasi ambayo alikuwa akiitumikia kabla ya kutua Yanga.

SOMA NA HII  BAADA YA DIRISHA LA USAJILI KUFUNGWA....MASTAA HAWA WA SIMBA NA YANGA KAZI WANAYO...

Inafahamika kwamba bosi wa GSM, Hersi Said ambao wamekuwa wakimwaga mamilioni kuisajilia Yanga, yupo Rwanda kwa mchakato huo wa mazungumzo na mabosi wa Kiyovu na asilimia kubwa mambo yanakwenda sawa ingawa akili ya tajiri wa Kiyovu ambaye naye ana fedha nyingi Nvukiyehe Jovenal ilikuwa ni kuwauza Uarabuni au Ulaya.

Juzi viungo hao walianza kuwaaga wachezaji wenzao wakiwaambia hawana muda mrefu wataondoka katika klabu hiyo huku wakigusia tu kuwa wanakwenda kucheza ndani ya Afrika hii kisha Ulaya baadaye.

Yanga wamepania kusuka kikosi cha kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa msimu ujao ambako wana uhakika wa kushiriki kutokana na kuongoza ligi mpaka sasa huku Tanzania ikipewa nafasi nne ya ushiriki wa kimataifa msimu ujao. Mashindano ya kimataifa msimu ujao yamepangwa kuanza kati ya Septemba na Oktoba mwaka huu. Yanga imejipanga kuhakikisha inaingia kwa nguvu kwenye mashindano hayo ili kuziba kejeli za Simba ambayo wamekuwa wakitambia rekodi zao zinazolibeba Taifa kimataifa.