Home Habari za michezo PAMOJA NA SIMBA KUTOLEWA SHIRIKISHO..MUGALU ANYOOSHEWA KIDOLE…MORRISON ATAJWA….

PAMOJA NA SIMBA KUTOLEWA SHIRIKISHO..MUGALU ANYOOSHEWA KIDOLE…MORRISON ATAJWA….


Ni wazi kwamba mshambuliaji Chris Mugalu ameigharimu Simba katika mchezo wa marudiano wa hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ugenini dhidi ya Orlando Pirates juzi Jumapili ambao walifungwa kwa penalti 4-3.

Kadi nyekundu ya dakika ya 58 ambayo mshambuliaji huyo alipata ilivuruga mipango ya Simba na kuilazimisha kufanya mabadiliko yaliyopunguza nguvu ya timu katikati na kuwapa mwanya Orlando Pirates kupata matokeo mazuri yaliyopelekea mechi hiyo kuamriwa kwa mikwaju ya penalti.

Kadi zote za njano ambazo Mugalu alizipata zilitokana na kukosa umakini na utulivu ambao ungemfanya kuziepuka kwa vile alicheza rafu ambazo hazikuwa na ulazima wa kufanya hivyo. Ilikuwa ni ngumu kwa Simba kukabiliana na Orlando Pirates huku wakiwa pungufu na hata mechi hiyo kwenda katika mikwaju ya penalti ilikuwa ni bahati kubwa kwao.

Pablo hana deni Simba

Kocha Pablo Franco alienda na mpango sahihi wa mechi kuikabili Orlando ambao kwa kiasi kikubwa ulifanikiwa kulingana na ubora wa wapinzani. Orlando ni timu ambayo imekuwa ikishambulia zaidi kutokea pembeni hasa kulia wakitumia zaidi mipira ya krosi za juu.

Kuanza na mabeki watatu wa kati na na beki Israel Patrick kama winga wa kulia ulikuwa ni mpango wenye lengo zuri la kuwadhibiti Pirates kimbinu na ulielekea kufanikiwa kwa kutoruhusu idadi kubwa ya mabao iwapo wangeshinda penalti.

Manula kadhihirisha

Kipa Aishi Manula amekuwa silaha ya Simba katika michezo mingi ugenini katika michuano hiyo kutokana na uwezo mkubwa wa kuokoa hatari ambao amekuwa akionyesha.

Hatari nne alizookoa jana za Orlando ambazo wange waliamini kuwa zingezaa mabao lakini pia penalti moja aliyookoa, ilikuwa ni muendelezo tu wa kuthibitisha daraja kubwa alilonalo kwa sasa kulinganisha na makipa wengine.

Orlando imepata darasa

Orlando imeingia hatua ya nusu fainali lakini namna walivyodhibitiwa na Simba katika mchezo wa juzi kinapaswa kuwaonyesha kuwa yapo maeneo wanayopaswa kuimarika zaidi ili waweze kufanya vyema katika hatua ya nusu fainali ambayo wataumana na Al Ahli Tripoli ya Libya.

SOMA NA HII  WAKATI ZOEZI LA USAJILI LIKIENDELEA...HAWA HAPA MASTAA 6 YANGA WATAKAOPIGWA PANGA...NDUGU WA AZIZ KI NDANI...

Safu yao ya ushambuliaji imekuwa na pupa na haina utulivu pindi inapokaribia lango la timu pinzani.

Pia wachezaji wake wamekuwa wakipendelea sana kuucheza mpira pindi wanapokuwa wanaumiliki kwa vile imekuwa ikiwapa mwanya wapinzani kujipanga.

Pengo Morrison

Katika mechi ambayo Simba walijipanga kushambulia kwa kushtukiza, walihitaji kuwa na mchezaji mbunifu na mwenye uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kasi kama Bernard Morrison.

Alishindwa kuwepo katika mechi ya juzi kwa vile alikuwa amezuiwa kuingia Afrika Kusini kutokana na kosa la kuvunja sheria ya uhamiaji ambalo aliyafanya siku za nyuma.

Ndiye kwa kiasi kikubwa aliamua mechi ya kwanza nyumbani kwa kusababisha penalti iliyowapa Simba bao pekee la ushindi lakini kukosekana kwake juzi, kulilinyima kitu benchi la ufundi la timu hiyo.

Simba iimarishe kikosi

Miongoni mwa mambo yamekuwa yakiikwamisha Simba robo fainali ni kutokuwa na kundi kubwa la wachezaji wa daraja la juu wanaoweza kuzitafsiri na kuzifanyia kazi vyema mbinu na mipango ya benchi la ufundi. Wapo wachache wanaoweza kufanya hivyo jambo linalomfanya Pablo na benchi lake kukosa watu mbadala wanaoweza kwenda kufanya kitu ndani ya uwanja ikiwa wale walioanza wameshindwa kuipa matokeo mazuri. Eneo la kwanza na muhimu ambalo Simba wanapaswa kuliimarisha ni lile la safu ya ushambuliaji.