Home Habari za michezo SIKU 100 TOKA AAJIRIWE SIMBA…HIVI NDIVYO AHMED ALLY ALIVYOJITOFAUTISHA NA MANARA…

SIKU 100 TOKA AAJIRIWE SIMBA…HIVI NDIVYO AHMED ALLY ALIVYOJITOFAUTISHA NA MANARA…


Ni mpole, uso wake haukauki tabasamu na akianza kuzungumza huwezi kuamini yanatoka mdomoni kwake, je unajua ni nani huyo? Ni Ahmed Ally, Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu ya Simba.

Aprili 15, 2022 alitimiza siku 100 za kufanya kazi na Simba, tangu ajiunge nao Januari 3 na amekuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na uwasilishaji wa ujumbe kwa mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo.

Mwanaspoti halikuwa nyuma kufuatilia anachokifanya Ahmed na limebaini kitu kilichomfanikisha kufanya kazi yake kwa ustadi na kukubalika mbele ya mashabiki.

TAALUMA INAMBEBA

Taaluma yake ya uandishi wa habari, inamrahisishia kufanya kazi na mashabiki wenye presha kubwa ndani ya kikosi hicho, tangu ajiunge nao anaonekana kuwapa raha.

Anapoisemea timu hiyo, anakuwa makini kuepuka kauli za kujitia kitanzi au kuishushia hadhi klabu hiyo kubwa nchini. Ahmed amekuwa anazungumzia zaidi mpira kuliko watu.

HANA POROJO

Anaepuka porojo katika majukumu yake, mfano alivyouzungumzia mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Orlando Pirates, alifafanua wamefunga bao 1-0 Kwa Mkapa, kulingana na ubora wa timu zilizofika hatua hiyo. Japo aliwasilisha ujumbe wake kwa utani na sauti utulivu, alizungumza kiufundi kwamba ni hatua ngumu inayotakiwa akili zaidi.

HATUMII NGUVU

Anapozungumzia jambo fulani kwenye timu yake, anakuwa kama hataki ila maneno yanayomtoka, asiyeipenda Simba anakuwa anakereka, huku wafuasi wake yakiwapa kicheko.

ANAJIWEKA KWA MASHABIKI

Ahmed sio mtu wa kufanya kazi kwa kukaa ofisini, amekuwa akionekana maeneo mbalimbali na mashabiki wa Simba, jambo linalozidi kutengeneza umoja na kuwafanya wajisikie vizuri kuona anawajali.   MTU WA WATU

Moja ya mambo aliyofanikiwa Ahmed ni kujiweka karibu na mashabiki wa timu hiyo na hilo limethihirishwa wakati wa maandalizi ya michuano mbalimbali ya Ligi Kuu Bara na ile ya kimataifa ambayo bila kujali cheo au heshima yake ameendelea kujichanganya na watu.

MSEMO WAKE MAARUFU

Kabla ya kuiduwaza Orlando Pirates kwenye mchezo wa kwanza hatua ya robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika, Ahmed aliibuka na msemo maarufu unaotamba kwa sasa: “Hawaamini macho yao”.

SOMA NA HII  KUHUSU KIPIGO CHA JANA ..MORRISON NAYE KAIBUKA NA YAKE HUKO...AFUNGUKA KWA HISIA KALI...

Akizungumzia siku 100 za uwepo wake madarakani, Ahmed alisema ni furaha kwake kuwepo kwenye klabu kubwa kama Simba na jambo alilofanikiwa japo si sana ni kuwaweka mashabiki karibu na timu yao.

“Bado nina malengo makubwa ya kuhakikisha timu inakuwa na shughuli nyingi kwa ajili ya kujipatia kipato, lakini pia tunatambua mashabiki ni mtaji hivyo nitaendelea kushirikiana nao ili timu yetu izidi kusonga mbele zaidi,” alisema mtangazaji huyo wa zamani wa vituo vya runinga vya Star Tv na Azam Tv kabla ya kutua Msimbazi.