MOHAMED Salah ameipa presha Liverpool baada ya kuumia kwenye mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA juzi usiku zikiwa zimebaki wiki mbili tu kabla ya fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya.
Nyota huyo wa Liverpool, alilazimika kutolewa uwanjani baada ya kuumia dakika ya 32 wakati mechi ikiendelea kwenye Uwanja wa Wembley akizua hofu kwa kocha wake Jurgen Klopp kutokana na umuhimu wake kikosini.
Salah alikaa chini akiwa na maumivu sehemu ya nyonga huku akizungukwa na wachezaji wenzake Thiago Alcantara na Sadio Mane kabla ya madaktari kuingia uwanjani kwaajili ya kumpa matibabu.
Baada ya Salah kutolewa uwanjani nafasi yake ikachukuliwa na Diogo Jota.
Kuumia kwa Salah huenda ikawa pigo kubwa katika kikosi cha Liverpool kuelekea fainali ya Ligi Mabingwa Ulaya dhidi ya Real Madrid, utakaochezwa Paris, Ufaransa Mei 28 mwaka huu.
Hii si mara ya kwanza Salah kutolewa uwanjani kutokana na majeraha kwani nyota huyo aliwahi kuumia kwenye mechi nyingine ya fainali lakini ya Ligi Mabingwa Ulaya Liverpool ilipolala mikononi mwa Real Madrid mwaka 2018.
Wakati huohuo, beki tegemeo wa Liverpool, Virgil Van Dijk alitoka uwanjani katika dakika ya 90 kabla ya mechi kuingia katika dakika 120 baada ya kuumia kufindo cha mguu.
Baada ya mechi kwisha kwa Liverpool kubeba ubingwa wa FA kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006 wakiifunga Chelsea kwa penalti 6-5, Van Dijk alisema alishindwa kuendelea na mechi kwasababu alisikia maumivu kwenye kifundo cha mguu.
“Nitaenda kwa daktari na kuangalia ukubwa wa tatizo, nilisikia maumivu wakati nacheza, sikutaka kuendelea kucheza kwa hofu.”