Kila mbabe na mbabe wake. Ndivyo unaweza kusema kwani wakati timu za Simba, Yanga na Azam zikijiuliza kwa Mbeya City, Coastal Union wao wameendelea kuitesa City kwa kuchukua alama sita msimu huu baada ya leo kushinda tena 1-0.
Msimu huu Mbeya City imeonesha ubabe kwa miamba ya soka nchini, Simba, Yanga na Azam kwa kuchukua alama nane ikiwa haijapoteza kwa vigogo hao ikiwa ni ushindi mechi mbili dhidi ya Simba (1-0) na Azam (2-2) mechi ya awali kisha kushinda 2-1 mchezo wa marudio na suluhu dhidi ya Yanga.
Pia Coastal Union wanakuwa timu pekee iliyoweka rekodi hadi sasa kwa kushinda dhidi ya Mbeya City nje ndani ambapo alama tatu za leo zimewafanya kuchumpa nafasi ya sita kwa pointi 34 baada ya mechi 26.
Katika mchezo wa leo uliopigwa uwanja wa Sokoine jijini hapa, licha ya timu zote kucheza kwa kasi na kutengeneza nafasi kadhaa, lakini umakini ulikosa kwa washambuliaji.
Wenyeji City watajilaumu zaidi kutokana na kukosa nafasi nyingi za wazi kupitia kwa Richardson Ng’ondya dakika ya 30 aliposhindwa kufunga bao akiwa na Kipa wa Coastal Union Mohamed Mohamed na Frank Ikobela dakika ya 37.
Wagosi nao walipambana kusaka bao la mapema lakini uimara wa mabeki na Kipa Deogratias Munish ‘Dida’ walikuwa wakali kutoruhusu hatari yoyote na kufanya timu hizo zinakwenda mapumziko kwa nguvu sawa ya bila kufungana.
Kipindi cha pili ndicho kilikuwa cha neema kwa Wagosi walipofanikiwa kupata bao dakika ya 46 kupitia kwa Vicent Aboubakari aliyeambaa na mpira na kuukwamisha mpira wavuni akimuacha Kipa Dida akisikitika na beki wake, Hamad Waziri.
Bao hilo lilionekana kuwachanganya City wakionekana kupaniki lakini baadaye walitulia na kushambulia japokuwa hawakuweza kuambulia kitu.
Kipigo hicho kinakuwa cha pili mfululizo kwa Mbeya City baada ya mechi iliyopita kulala 3-0 dhidi ya KMC huku wakiruhusu idadi kubwa ya mabao manne.
Tukio la kushangaza baada ya mechi hiyo, mashabiki walimsubiri kwa Kocha Mkuu, Mathias Lule wakimtolea maneno makali huku Jeshi la Polisi likimuwekea ulinzi mkali hadi kumsindikiza kutoka uwanjani.