PABLO Franco,Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa haelewi namna mambo yanavyokwenda kwenye timu hiyo hasa katika safu ya ushambuiaji.
Simba imekuwa kwenye mwendo wa kusuasa msimu huu wa 2021/22 ipo kwenye nafasi ya kupoteza ubingwa wao wa ligi ambao wanautetea kwa kuwa wameachwa zaidi ya pointi 10 na wapinzani wao Yanga.
Ikiwa ipo nafasi ya pili,Simba imekusanya pointi 51 baada ya kucheza mechi 25 huku vinara wakiwa ni Yanga wenye pointi 64.
Sare ya kufungana bao 1-1 dhidi ya Geita Gold ilimvuruga Pablo ambaye ameweka wazi kwamba alipoteza mchezo huo kutokana na makosa ya safu ya ushambuliaji.
“Sijui jambo gani ambalo ninaweza kufanya kwa sasa hasa ukizingatia kwamba tunatengeneza nafasi nyingi na tunashindwa kuzitumia hilo linatufanya tunashindwa kupata matokeo.
“Hakuna namna tutafanyia kazi makosa ambayo yametokea ili kuweza kurejea kwenye ubora kwa mechi zetu zijazo lazima tufanye vizuri,” amesema Pablo.
Kwa sasa timu ipo Mwanza ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo wa Kombe la Shirikisho hatua ya nusu fainali dhidi ya Yanga unatarajiwa kuchezwa Mei 28, Uwanja wa CCM Kirumba.