Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI YAO NA YANGA LEO…MASTAA SIMBA WAVUNJA UKIMYA…WAFUNGUKA HALI ILIVYO KWENYE...

KUELEKEA MECHI YAO NA YANGA LEO…MASTAA SIMBA WAVUNJA UKIMYA…WAFUNGUKA HALI ILIVYO KWENYE TIMU…


Baada ya uongozi wa Simba kufanya kikao cha ndani kwenye kambi ya timu jijini Mwanza siku tatu kabla ya mchezo wa nusu fainali Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Yanga, hali na morali imerejea tofauti na hapo awali.

Kabla ya kikao morali ya Simba ilionekana kuwa chini kutokana na kucheza michezo sita huku wakipata ushindi mmoja dhidi ya Ruvu Shooting na minne kutoka suluhu.

Nahodha wa Simba, John Bocco na straika Kibu Denis wamewaambia mashabiki kwamba wamewasikia kiu yao na wanajua cha kufanya kwenye mchezo ujao.

Bocco alisema kuwa atazungumza na wenzake pamoja na kuhamasishana ili kila mmoja atakayepata nafasi ya kuiwakilisha timu dhidi ya Yanga apambane hadi jasho lake la mwisho na kufanikisha lengo la kushinda.

Alisema Kombe la ASFC lipo mikononi mwao ni uamuzi wao waweze kulibakisha kwa maana ya kufanya vizuri.

“Tunayo nafasi ya kulibakisha kombe hili au tuliache liende kwa timu nyingine kikubwa ambacho naamini tunakwenda kupambana ili tufanye vizuri,” alisema Bocco mwenye mabao matatu kwenye ligi.

Msimu uliopita Simba ilitwaa ubingwa baada ya kushinda bao 1-0 kwenye fainali dhidi ya Yanga iliyochezwa Kigoma.

Kibu Denis alisema: “Kushinda mechi kubwa ya namna hii ina maana kubwa kwetu kama timu tunakaribia kufikia malengo pamoja na wachezaji kufanikisha kile ambacho hata mashabiki wetu wanatamani kukiona, tunaenda kupambana.” Kibu amefikia rekodi yake ya msimu uliopita ya kufunga mabao saba kwenye ligi.

“Kuhusu kiwango changu hakuna siri nyuma yake zaidi ya kujituma na kupambana kuona Simba inafanikiwa ndio maana hayo mengine yanakuja imani yangu naweza kuvunja rekodi ya msimu uliopita kwa maana ya kufunga mabao mengi zaidi ya haya.” Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alisema hali ya matokeo katika kikosi chao hivi karibuni haikuwa nzuri ila kwenye mechi ijayo inaweza kuwa tofauti.

“Tumezungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi kila mmoja kwa nafasi yake kusahau yaliyotokea nyuma nguvu na akili kuweka katika mechi dhidi ya Yanga ambayo tuna kila sababu ya kupata ushindi,” alisema Barbara ambaye yupo na timu kambini Mwanza.

SOMA NA HII  ALLY KAMWE ATAMBA , MUSONDA AZIDI KUNOGA

Jana jioni Simba ilipasha kwenye Uwanja wa Nyamagana chini ya ulinzi mkali ambapo hakuruhusiwa mtu isipokuwa wachezaji, benchi la ufundi au kiongozi. Ulifanyika ukaguzi mkali wa makomando kuangalia kona moja baada ya nyingine kuhakikisha hakuna mamluki aliyebaki ndani ya uwanja au anayechungulia mpaka wakamaliza jambo lao.