Home Habari za michezo NNJE YA DIMBA:..SIMBA NA YANGA WASIPOTUMIA NJIA HIZI KUTOBOA CAF,.. WATAISHIA KUFA...

NNJE YA DIMBA:..SIMBA NA YANGA WASIPOTUMIA NJIA HIZI KUTOBOA CAF,.. WATAISHIA KUFA KIUME…

Habari za michezo

Hali imechafuka. Dakika 180 za Simba na Yanga kwenye mechi za hatua ya makundi, zimetoa picha tofauti na iliyokuwa ikidhaniwa awali. Hivyo,kimahesabu ni kwamba watahitaji pointi 10 ili kuwa salama. Sambamba na kufuzu robofainali.

Timu hizo wikiendi ijayo zitakuwa ugenini kusaka angalau ushindi wa kwanza kimataifa msimu huu.

Simba inatakiwa kukusanya pointi saba kwenye michezo minne iliyobaki ili iwe na matumaini ya kufuzu kwa hatua hiyo, lakini itawalazimu pia kuhesabu vidole. Mazungumzo ya wengi yamekuwa yakiwaaminisha mashabiki wa soka kuwa timu zikifikisha pointi tisa zinafuzu. Lakini kimahesabu, timu inaweza kufikisha tisa na bado isifuzu, lakini pia inaweza kufikisha idadi hiyo na kufuzu moja kwa moja.

Yanga bado wamebakiza michezo miwili ugenini dhidi ya Medeama pamoja na Al Ahly, lakini miwili nyumbani dhidi ya Medeama na CR Belouzidad.

Katika michezo miwili ya kwanza, Yanga walilala mabao 3-0 kwa Belouzidad, lakini wakatoka sare ya bao 1-1 na Ahly jambo ambalo limewafanya kukusanya pointi hiyo moja.

KIMAHESABU:

Yanga ili iwe na matumaini ya kufuzu, inatakiwa kushinda michezo miwili dhidi ya Medeama na kufikisha pointi saba, lakini pia ipate ushindi dhidi ya Belouzidad kwenye Uwanja wa Mkapa ambapo itafikisha pointi kumi kwa asili ya kundi itakuwa kwenye wakati mzuri.

Kimahesabu, Yanga itakuwa imejiweka kwenye nyakati nzuri za kufuzu hatua ya robo fainali na itakwenda Misri kumalizana na Ahly bila presha.

Wakati Yanga inacheza na Medeama, kumbuka kuwa Ahly itakuwa ikimalizana na Belouizdad kwenye michezo ya nyumbani na ugenini, kama Ahly itafanikiwa kushinda michezo yote itakuwa imefikisha pointi kumi, ikiwa na uhakika wa kwenda robo, kimahesabu.

Lakini itakuwa imebakiza mchezo dhidi ya Medeama ugenini na Yanga nyumbani ambapo kwa uhakika wa kuongoza kundi itatakiwa kutafuta pointi tatu.

Lakini kama watagawana pointi na CR, kila mmoja akachukua tatu hali hiyo itawalazima Ahly kushinda dhidi ya Medeame ugenini na kufikisha pointi 10 halafu ili wawe na uhakika wa uongozi kwenye kundi itatakiwa kuwafunga Yanga na kufikisha pointi 13, ambapo poa mahesabu yao yatakuwa kwa CR.

KOSA MOJA:

Kwa hali ilivyo, kama Yanga itashindwa kukusanya pointi zote sita kwenye michezo yake miwili dhidi ya Medeama, ikapoteza ugenini na kushinda nyumbani, itakuwa na pointi nne na Medeama saba.

Haya yatakuwa matokeo mazuri kwa Medeama kwa kuwa pointi zao saba zitawalazimisha kutafuta pointi tatu kwenye michezo miwili, dhidi ya Ahly na Belouzdad na kufikisha kumi ambazo zitakuwa zinawapeleka na Yanga itatakiwa kuichapa Ahly na Belouzdad na kufikisha pointi 10 ambazo zitawafanya waangalie walipokutana ‘head to head’.

Hii ina maana kuwa Yanga matumaini yao ya kufuzu ni kufikisha pointi 10 kwa jinsi kundi lao lilivyo, sehemu ambayo kutakuwa na kizingiti kidogo sana wao kufuzu.

SIMBA MTIHANI:

Simba kimahesabu inadaiwa pointi saba ili kufikisha tisa,lakini uhakika wanatakiwa kutafuta pointi nane kwenye michezo minne iliyobaki ambayo ina pointi 12 ili irudi kwenye hatua ya robo fainali.

Jambo la kwanza kwa Simba ni kukusanya pointi sita kwa Wydad AC ambao hawana pointi, wamepoteza mchezo nyumbani na na ugenini, ambapo itafikisha pointi nane na kukusanya mbili kwenye michezo miwili, aidha itoke sare dhidi ya Asec na Jwaneng Galaxy kwenye Uwanja wa Mkapa.

Au mahesabu mengine kwa Simba inatakiwa kushinda miwili dhidi ya Wydad na kushinda mmoja dhidi ya Jwaneng ambapo watakuwa na pointi 11 zinazoweza kuwavusha moja kwa moja.

Lakini jambo la ajabu ni kwamba, wakati Simba inafikiri kuhusu ushindi kwa Wydad, Asec na Jwaneng ambao mpaka sasa wana nafasi kubwa ya kufuzu kila moja ikiwa na pointi nne, matokeo yao kwenye michezo miwili wanayokutana inaweza kuipa mwanga zaidi Simba au kuiangamiza kabisa.

Matokeo mazuri kwa Simba ni sare michezo yote miwili, kama timu hizo zitatoka sare michezo yote ina maana kuwa zitakuwa na pointi sita kila moja na Simba kama ikishinda yote miwili ya Wydad itakuwa na pointi nane, lakini kama kila moja itashinda kwake, zitafikisha pointi saba saba ambapo kila mmoja michezo ya mwisho itakuwa vita kwake.

Lakini kama Simba ikipata ushindi kwenye mchezo mmoja dhidi ya Wydad, itakuwa na pointi tano na itakuwa inalazimika kushinda michezo yote miwili iliyobaki, ili ifikisha pointi 11 na kufuzu, kama itashinda mmoja na kupata sare mmoja itakuwa na pointi tisa ambazo zitategemea zaidi matokeo ya timu nyingine kufuzu, hali ambayo kwa asili ya matokeo ya kundi inaonekana kuwa ngumu kwao.

POINTI 9 ZA KISHABIKI:

Kumekuwa na kauli mbalimbali zinaonyesha kuwa timu ikifikisha pointi tisa inakuwa na uhakika wa kufuzu, lakini kimahesabu siyo sawa, kwa asili ya kundi kama la Simba zaidi ya timu tatu zinaweza kufika idadi hiyo.

Asec ikishinda mchezo mmoja dhidi ya Galaxy na Galaxy ikashinda mmoja, zote zitakuwa na pointi saba na zitabakiza michezo miwili, halafu Simba ikaibuka na ushindi kwenye michezo miwili dhidi ya Wydad itakuwa imefikisha pointi nane.

Simba ikaibuka na ushindi dhidi ya Galaxy itafikisha 11, Asec wakaibuka na ushindi dhidi ya Wydad itakuwa na 10 na Galaxy wakaibuka na ushindi dhidi ya Asec watakuwa na pointi 10, kimahesabu pointi tisa siyo uhakika wa kufuzu kwenda robo fainali.

REKODI ZINASEMA:

Msimu wa 2022/2023 kundi B, Mamelodi ilikusanya pointi 14, Al Ahly ilikusanya pointi 10 na Al Hilal 10, zilienda robo fainali, Mamelodi na Ahly, Hilal walibaki na pointi zao kumi.

Pia msimu wa 2019/2020, Kundi B, Etoile du Sahel walikuwa na pointi 12, Al Ahly pointi 11 na Al Hilal 10 lakini wakaenda wawili Hilal akabaki.

Lakini kwa wale wanaoamini pointi tisa timu inafuzu, msimu wa 2020/2021 Kundi C, Wydad ilikuwa na pointi 13, Kaizer Chiefs ilikuwa na pointi tisa, Horoya tisa, lakini zilienda Wydad na Kaizer, hivyo pointi tisa pia siyo kigezo cha moja kwa moja cha kufuzu.

UJUMBE WA YANGA:

Nahodha na beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Canavaro’ akizungumza na Mwanaspoti kutoka Marekani ambako anaishi kwasasa, alisema wachezaji wa Yanga wazingatie heshima, utulivu na kujitoa wawapo uwanjani kucheza na timu kubwa hasa zinazoshiriki michuano hiyo mikubwa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Ukiangalia kwa haraka uwaweza kusema safari ndo imefika mwisho, kutokana na aina ya uchezaji wa wachezaji wa Yanga, wanapaswa kubadilika wakiwa wanacheza na timu kubwa hasa mashindano haya.

“Ni kuzingatia heshima kwa maana ya kumheshimu mpinzani wako, utulivu na kujitoa binafsi, timu kama Mediama sio wa mchezo mchezo, wanapaswa kujipanga,” alisema Canavaro ambaye pia amewahi kuwa mchezaji wa Taifa Stars na meneja wa timu hiyo.

Kuhusu uzoefu wa wachezaji wa Yanga kwenye michuano hiyo, Canavaro alisema; “Yanga ni timu kubwa, sisi tuliwafunga hapo hapo kwa Mkapa, hivyo uzoefu isiwe sababu.”

Ikumbukwe kuwa, Machi 2014, Yanga iliifunga Al Ahly bao 1-0 kwenye uwanja huo na michuano hiyo hiyo, bao pekee la Yanga lilifungwa na Canavaro dakika ya 83 akifunga kwa kichwa baada ya kuunganisha mpira wa kona iliyopigwa na Simon Msuva.

SIMBA MATUMAINI:

Ofisa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema; “Nafasi yetu kwenda robo fainali bado ipo wazi na tutaanza kuthibitisha hilo kwenye mechi ijayo dhidi ya Wydad.”

Simba inapaa leo usiku kwenda nchini Morocco, itakiwasha na Wydad AC Jumamosi saa 4:00 usiku.

Hata hivyo safari hiyo ya zaidi ya masaa matano ambayo itailazimu Simba kupanda ndege mbili hadi tatu tofauti ni ya kimkakati zaidi ambapo Kocha mkuu mpya wa kikosi hicho, Mualgeria Abdelhak Benchikha ndiye amependekeza timu kuwahi ili ijiandae na walau kwa siku mbili. Tupe maoni yako pointi 10 zitapatikana?

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  MECHI ZA USHINDI LEO ZIMELALA NA ODDS HIZI KUTOKA MERIDIANBET...