Home Habari za michezo MASAU BWIRRE:- UCHAWI UPO JAMANI….TAIFA STARS WASHAWAHI KUSAFIRI NA ‘WAGANGA’ 12 IKAISHIA...

MASAU BWIRRE:- UCHAWI UPO JAMANI….TAIFA STARS WASHAWAHI KUSAFIRI NA ‘WAGANGA’ 12 IKAISHIA KUPIGWA GOLI 7-0…


NA Masau Bwirre.

USHIRIKINA na uchawi katika soka la Tanzania kama siyo Afrika unafanyika karibu timu zote – iwe klabu au timu za Taifa ni kawaida wote wanaamini bila kujishughulisha no ni vigumu kumshinda mpinzani.

Imefikia hatua katika klabu za soka uwezo wa wachezaji hauaminiwi na ili ushinde lazima ndumba zitumike. Huko tuendako usishangae klabu kuajiri waganga wa kutosha kwa kazi hiyo.

Kipindi cha nyuma walifanya shughuli za ulozi kwa kificho, lakini sasa kwa kuona ni sehemu ya mafanikio na ushindi wapo wanaofanya hadharani – mchana kweupe mashabiki na watazamaji wanashuhudia. Ni uongo tu akitokea mtu, kiongozi au shabiki wa klabu fulani, anajipiga kifua akidai klabu yake haishiriki vitendo vya kishirikina na uchawi huyo ni mnafiki. Anajaribu kujikosha na kujificha kwenye uongo, lakini ukweli ni kwamba wanafanya na anajua kwamba hata klabu yake inakimbizana makaburini kuusaka ushindi kupitia ‘wataalamu’.

Mara kadhaa tumeshuhudia baadhi ya klabu na wachezaji kuingia uwanjani kupitia mlango usio rasmi, gari la wachezaji na wachezaji wenyewe kuingia uwanjani kinyumenyume na mengi tu yasiyo ya kawaida kufanyika kabla na wakati wa mchezo.Usidhani hayo ni staili tu, ni maelekezo ya sangoma kwamba, kwa kufanya hivyo ushindi utapatikana. Katika mwendelezo wa makala maalumu kuhusu masuala ya ushirikina na uchawi katika soka kupitia safu hii baada ya kueleza namna wachezaji, waamuzi, timu na klabu za soka wanavyoshiriki mambo hayo, leo nataka nigusie kidogo matukio machache ya aina hiyo yaliyowahi kuigusa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ miaka ya nyuma.

Hii ni kuonyesha ambavyo wakati fulani mazingira na tamaduni vinavyolazimisha kufanyika kwa jambo fulani kwa imani ili mafanikio yapatikane. Katika soka la Afrika moja ya nchi iliyopiga hatua na ina mafanikio makubwa kisoka ni Misri, lakini unaweza ukaamini kwamba pamoja na mafanikio hayo Misri wanaamini na wanashiriki vitendo hivyo? Miaka ya nyuma Taifa Stars ilipangwa kucheza na timu ya Taifa ya Misri kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia mchezo uliochezwa usiku katika mji wa Alexandria.

Uchunguzi wangu na maelezo niliyopata kutoka kwa mmoja wa maofisa waratibu waandamizi wa Stars, mchezo huo walishuhudia vitendo vya kishirikina na uchawi vikifanywa na wenyeji hadharani mbele yao.

Alisema wakati Stars wanaelekea uwanjani wakiwa katika geti la kuingilia ilitokea gari aina ya Fuso iliyokuwa imebeba ngamia (mnyama) ikalizuia kwa mbele basi walilokuwa wamepanda wachezaji na viongozi.

Baada ya msafara wa Taifa Starts kuzuiwa, wenyeji hao walishusha ngamia na kumchinja hadharani kwa kutumia mashine ya kuchinjia wanyama mbele ya wachezaji na viongozi wa Stars. Viongozi wa Stars walioambatana na timu walioshuhudia tukio hilo walitaka pamoja nao, wachezaji wote washuke kwenye hilo basi ili watumie milango ya kawaida kuingia uwanjani kukwepa kukanyaga damu iliyotapakaa getini na mbele ya gari lao. Dereva wa basi lililowabeba wachezaji na viongozi wa Stars alikataa kufungua mlango wa basi, hivyo akawapitisha katika geti hilo kwenye damu za ngamia.

Tukio hilo liliwanyong’onyesha na kuwatoa mchezoni wachezaji wa Stars ambapo matokeoni kuwa ilichapwa mabao 4-0. Baada ya tukio hilo, ulozi wa kuchinja ngamia mmoja wa maofisa anasema viongozi wa timu hiyo wakati huo walipata somo na kuchangamka mechi zilizofuata walijiongeza na kuweka mambo sawa ‘wataalamu’ walishirikishwa katika kuusaka ushindi.

Anasema wakati Stars inajiandaa kwenda kucheza na Malawi ambapo walisafiri kwa ndege ya kukodi alikabidhiwa na viongozi wake mtu mmoja wa makamo na kuambiwa kwamba huyo ni mtaalamu wa timu na ahakikishe anasafiri kwa ndege.

Anasema alipomuomba hati ya kusafiria mtaalamu huyo alisema hana na akasema hasafiri kwa ndege, ila wasiwe na wasiwasi watamkuta Malawi. “Tuliondoka tukamuacha mtaalamu huyo Dar es Salaam mwendo wa ndege kutoka Dar es Salaam hadi Lilongwe-Malawi ni takribani saa mbili. Tulitua uwanja wa ndege wa Lilongwe saa 2.00 usiku nilishangaa kumkuta mtaalamu huyo uwanjani hapo akitusubiri na kutupokea,” alisema ofisa huyo.

SOMA NA HII  SAFARI YA UKAME WA MIAKA 25 KWA YANGA NDANI YA CAF KUVUNJWA RASMI LEO....KAA MKAO WA KULA...

Anaeleza kuwa mchezo huo ulipangwa kuchezwa Blantyre, hivyo waliondoka Lilongwe saa 3.00 usiku kuelekea Blantyre umbali wa kilomita 400 kutoka Lilongwe kwa njia ya barabara, lakini mtaalamu ambaye hakupanda basi lililowabeba wakamkuta tayari ni mwenyeji Blantyre.

Wenyeji waliandaa Stars ifikie katika Hoteli ya Victoria Blantyre, lakini kwa kuogopa na kuhofia mambo yetu, ubalozi wa Tanzania uliandaa hoteli nyingine – Malawi Sun ambapo ndipo walipofikia wachezaji. Hoteli ya Victoria Blantyre walifikia waandishi wa habari, baadhi ya viongozi na mtaalamu ambaye aliomba apatiwe chumba kwenye kona.

Baada ya kikao cha maandalizi ya mchezo uongozi wa Starts ulikabidhiwa funguo za chumba ambapo mtaalamu aliyefanywa kama mmoja wa maofisa wa timu walikwenda kukikagua chumba hicho. Katika ukaguzi wa chumba mtaalamu huyo alidai kimechafuliwa, hakifai na akatoa maelekezo timu isiingie chumbani.

Mtaalamu huyo ambaye inasemekana alitokea Mafinga – Iringa alikuwa na kijichupa na ndani yake kulikuwa na maji aliyonyunyiza kwenye hicho chumba ukafuka moshi uliowakusanya walinzi wa uwanja wakidhani kuna moto. Mtaalam alidai moshi huo ni sehemu ya uchafu uliokusudiwa kuwafanya wachezaji wetu uwanjani waone moshi badala ya mpira. Maelekezo ya mtaalamu yalizingatiwa na kufuatwa – kweli Stars haikuingia kwenye chumba cha kubadilishia mavazi ambazo walibadilishia kwenye gari.

Wakati wa mechi, mtaalamu aliomba akae kwenye jukwaa la VVIP na akaomba awe karibu na ofisa mratibu mwandamizi wa Stars, ambapo ililazimika ofisa aliyewahi kuwa msaidizi wa rais wa TFF wakati huo tiketi yake anyang’anywe kwa kisingizio cha kupewa ofisa ubalozi, ila akapewa mtaalamu huyo.

“Nikiwa nimekaa jirani na mtaalamu huyo jukwaa la VVIP, alipita mzee mmoja amevaa kanzu nyeupe, mkononi ameshika mkuki, mgwisu na kamba fulani hivi ya shanga. Ghafla nilijisikia kizunguzungu, nikawa kama naelea juu, wachezaji uwanjani nikawa nawaona kwa chini. Nilipozinduka Malawi wanashangilia goli,” anasema ofisa huyo.

Anasema wakati Malawi wanashangilia goli hilo, mtaalamu alimwambia kwamba hilo ni goli pekee katika mchezo huo uliohudhuriwa na Rais wa Malawi wakati huo, Joyce Banda na halitafungwa jingine na timu yoyote, na kwamba ilikuwa Starts ifungwe magoli matatu na mawili tayari ameyatengua.

Stars ilishambuliwa wakati fulani mshambuliaji wa Malawi anabaki yeye na goli, lakini anashindwa kufunga na mtaalam alikuwa akiinama na kuinuka, mpira unapaa juu ya lango au unabutuliwa. Siku ya kuondoka mtaalamu bado alikataa kupanda ndege, akasema atarudi Dar es Salaam kama alivyokwenda Malawi. Amini usiamini wakati ndege inatua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere mtaalamu alikutwa anakunywa chai kwenye mgahawa uwanjani hapo.

Tukio jingine ni Stars ilipocheza na Algeria katika mji wa Algers. Katika kuhakikisha timu yetu haichezewi mchezo mchafu kama ule wa Misri, wataalamu 12 walipanda ndege kwenda Algeria kuimarisha ulinzi na kuusaka ushindi.

Kilichotokea katika mchezo huo Starts ilifungwa magoli 7-0 ikaonekana kuzidiwa kila eneo na kila idara. Baada ya mchezo Stars ilipaswa kuondoka na ndege ya saa 11.00 alfajiri kurudi Dar es Salaam, lakini cha ajabu msafara mzima wachezaji, viongozi na waandishi wa habari, walizidiwa na usingizi wote kwa pamoja wakazinduka saa 2.00 asubuhi isipokuwa kiongozi wa wataalamu ambaye naye hakuamka hadi alipoamshwa, hivyo wakaachwa na ndege.

Hii ilitafsiriwa kwamba utaalamu wa wataalamu wa Algeria ulikuwa wa hali na viwango vya juu kuliko wataalamu 12 wa Stars, hivyo msafara wake ulileweshwa na kuchoshwa na kutegeshewa muda wa kuamka kwa pamoja.

Hali hiyo ilisababisha wachezaji na viongozi wa Stars wasafiri kwa mafungu kwa kuwa tiketi zilikatwa upya na hazikupatikana za kuwatosha wote kusafiri pamoja. Ushirikina na uchawi katika soka upo na wengi wanaushiriki na hata viongozi kwenye mpira ngazi mbalimbali wengi wao wanafanya, japo kwa malengo tofauti.

Ushauri wangu niwasihi wasiendekeze ushirikina na uchawi, bali wajiandae katika ubora na uwezo, zaidi sana wamtegemea Mungu.

Makala haya yalichapishwa kwanza kwenye wavuti la MwanaSpoti