Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU….YANI BADO WATU WANAAMINI GEORGE MPOLE NI ‘CHIPUKIZI’…KIBWANA ANAWEZA KUCHEZA ULAYA….?

UKWELI MCHUNGU….YANI BADO WATU WANAAMINI GEORGE MPOLE NI ‘CHIPUKIZI’…KIBWANA ANAWEZA KUCHEZA ULAYA….?


Ilipokufa Ze Komedi Shoo. Ilivyokufa Orijino Komedi. Ilivyokufa Futuhi. Nikadhani vichekesho vimeisha Tanzania. Kumbe ndio kwanza vimehamia kwenye soka. Ni ajabu na kweli.

Ni rasmi sasa vichekesho vimehamia kwenye soka letu. Viongozi ni vichekesho. Wachambuzi ni vichekesho. Wasemaji ni vichekesho na wachezaji pia wamekuwa hivyo hivyo.

Baada ya kupotea kwa mafuta ya Kimbo nikadhani akili Mgando zitakuwa zimekwisha nchini. Kumbe zimeamia kwenye soka. Waandishi wa habari na wachambuzi wengi wamekuwa na akili mgando. Viongozi pia wana akili mgando. Yaani vurugu tupu.

Leo hii utasikia Waandishi wa Habari, Wachambuzi, Viongozi wa soka wakizungumza kuhusu hatma ya timu yetu ya Taifa. Wote watakwambia suluhu ya tatizo letu ni wachezaji kwenda kucheza soka nje ya nchi. Lakini hakuna anayesema nani aende?

Nje ya nchi siyo kama choo cha baa ama soko kwamba kila mtu anaweza kwenda.

Soka la wenzetu ni kazi kwa Wanaume wa shoka. Ili ucheze soka nje hasa nchi za Afrika Kaskazini na Ulaya lazima uwe na kipaji cha kweli. Halafu uwe mtu wa mazoezi.

Huyo Mbwana Samatta na kujua kwake soka alilazimika kucheza soka la Afrika kwa kiwango cha juu kwa miaka Zaidi ya minne ndipo akaenda Ulaya.

Huwezi kuamka tu asubuhi na kwenda Ulaya kama unavyokwenda kwa Shangazi yako pake Buza. Ulaya ni Sayari nyingine.

Lazima tuwe wakweli katika nafsi zetu ndipo tuweze kuusaidia mpira wetu.

Hatuwezi kuwa na timu imara ya Taifa kwa kutaka kupeleka wachezaji wa ovyo Ulaya. Lazima tupeleke wachezaji imara katika umri sahihi.

Nakumbuka wakati wa mechi za kirafiki za Kimataifa mwezi Machi mwaka huu, Kocha wa Taifa Stars, Kim Paulsen alimsifu George Mpole kama mchezaji chipukizi anayekuja vizuri. Inachekesha sana. Leo Mpole kawa Chipukizi?

Ukitazama kidevu cha Mpole amenyoa ndevu mara nyingi pengine kuliko mimi. Mpole ameanza kucheza soka la ushindani tangu mwaka 2015, leo anakuwaje chipukizi? Hii ndio Tanzania iliyojaa maajabu.

Mchezaji wa Tanzania hawezi kucheza soka kwa miaka saba na bado akawa chipukizi. Tunajuana.

Utasikia baadhi ya watu wakisema sasa ndio muda muafaka kwa Mpole kwenda kucheza soka nje ya nchi. Huu sasa ndio uongo wenyewe. Mpole ameshachelewa kwenda huko Duniani. Kwa miaka yake ya kweli, anatakiwa asaini Mkataba Simba ama Yanga maisha yaendelee.

Hao wanaokwambia Mpole aende kucheza nje ya nchi ndio hao mpaka leo wanaamini kuwa Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ bado ni mchezaji kijana. Inachekesha sana. Tshabalala anacheza soka la ushindani kwa miaka 10 sasa, anakuwaje kijana?

SOMA NA HII  KISA KUACHWA NA SIMBA ...DILUNGA AVUNJA UKIMYA...AFUNGUKA A-Z KUHUSU MKATABA WAKE...'BWALYA' ATIA NENO....

Ndio hao hao wanaamini kuwa sasa ni umri sahihi kwa Aishi Manula kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi. Manula alidaka mechi yake ya kwanza ya mashidano mwaka 2013. Ilikuwa Ngao ya Jamii kati ya Yanga na Azam FC. Inakuwaje leo ndio iwe muda wake muafaka kwenda nje? Ni kichekesho. Muda wake ushapita.

Tatizo Watanzania wengi tumejaa mihemko na uongo mwingi. Hatutaki kusema ukweli.

Majuzi nimeona beki wa Yanga, Kibwana Shomary amesaini mkataba mpya.

Kuna baadhi ya watu wanasema ilikuwa muda sahihi kwa Kibwana kuondoka kwenda kucheza soka la kulipwa nje. Uongo ulioje.

Ni kweli tunataka hawa kina Kibwana waende nje ya nchi, lakini siyo kwa namna tunayotaka sisi. Kibwana ni beki wa kulia.

Amekaa pale Yanga kwa misimu miwili sasa. Msimu uliopita Yanga waliona hatoshi katika nafasi hiyo na kuamua kumsajili Djuma Shaban.

Kwa kifupi ni kwamba Djuma ni mzuri kuliko Kibwana.

Hii ndiyo sababu ili Kibwana aanze kikosi cha kwanza sasa lazima acheze beki ya kushoto. Amehamishwa nafasi. Sasa kama Djuma anamzidi Kibwana ubora, unataka aende nje ipi? Ili Kibwana aende nje ya nchi lazima awe bora kwanza hapa nchini.

Inabidi amuweke Djuma benchi pale Yanga. Halafu amuweke Shomari Kapombe benchi pale Taifa Stars.

Hapo tutaseme Kibwana sasa anaweza kwenda nje akaimarike Zaidi. Sasa mchezaji hana uhakika wa nafasi kwenye Ligi yetu, huko nje ya nchi tunataka akafanye nini?

Hii ndiyo sababu wapo baadhi ya wachezaji waliokwenda nje kama Eliuter Mpepo, Eliud Ambokile, Ramadhan Singano na wengineo lakini hawajawahi kuwa na msaada wowote kwa Taifa Stars. Kwanini? Ni kwasababu ni wachezaji wazuri wa kawaida. Siyo wachezaji mahiri.

Njia za kupeleka wachezaji nje ya nchi ziko mbili tu. Kwanza, ni kuchukua wachezaji mahiri katika umri mdogo.

Mfano mzuri ni yule Kelvin John. Amekwenda Ulaya katika umri sahihi. Miaka mitatu ijayo anaweza kuwa staa wa Taifa Stars.

Njia ya pili ni kupeleka wachezaji wetu mahiri nje ya nchi. Mfano mzuri ni namna Saimon Msuva aliondoka. Alicheza kwanza hapa na kuwa katika kiwango bora. Alikuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu mara mbili kabla ya kwenda Morocco. Alishazoea changamoto zote za hapa.

Ndio sababu Msuva alifanikiwa pale Morocco. Ndiyo sababu amekuwa msaada pale Taifa Stars. Ila kwa kutaka kupeleka wachezaji wa mchongo nje, tutaendelea kubaki palepale.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here