YANGA ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa Mzambia, Lazarous Kambole, anayekipiga Klabu ya Kaizer Chiefs ya nchini Afrika Kusini.
Hiyo ni katika kukiimarisha kikosi chao katika kuelekea michuano ya kimataifa msimu ujao ambao Yanga ina asilimia 99 ya kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga imepanga kufanya usajili babkubwa kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu na viwango bora katika msimu ujao.
Kwa mujibu wa taarifa Yanga imefikia makubaliano binafsi na mshambuliaji huyo ambaye hana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Chiefs.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa mshambuliaji huyo anaondoka Chiefs kama mchezaji huru kutokana na mkataba wake kumalizika mwezi huu.
Aliongeza kuwa wakati wakijiandaa kukamilisha usajili wa mshambuliaji huyo, Yanga ipo katika mazungumzo na baadhi ya wachezaji wengine wa kigeni akiwemo Mghana, Bernard Morrison aliyemaliza mkataba wake Simba.
“Tumeanza mazungumzo binafsi na Kambole na hivi sasa tupo katika hatua za mwishoni za kufikia makubaliano binafsi ya kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa katika kuiboresha safu ya ushambuliaji.
“Tutamsajili Kambole kama mchezaji huru, kwani mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu na hii itakuwa mara ya pili kwa Yanga kumfuata Kambole.
“Awali, tulishindwa kufanikisha usajili wake kutokana na kubanwa na mkataba ambao ulikuwa mrefu, lakini hivi sasa tuna nafasi ya kumsajili kutokana na kufikia makubaliano mazuri,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mjumbe wa Kamati ya Mashindano wa Yanga na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM, Injinia Hersi Said, alisema: “Usajili ni siri ya klabu hivi sasa, lakini utakapokamilika tutaweka wazi, kwa kifupi tumepanga kufanya usajili mkubwa wa kuleta wachezaji wa daraja la juu.”