TIMU ya taifa ya Algeria imeendelea kuonesha ubabe kwenye kundi F kuwania kufuzu fainalo za mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya kuichapa Tanzania ‘Taifa Stars’ mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Huo umekuwa ushindi wa pili mfululizo kwa Algeria baada ya kushinda mechi ya kwanza dhidi ya Uganda na sasa imefikisha alama sita na kuongoza kundi F ikifuatiwa na Niger yenye mbili huku Tanzania na Uganda kila moja ikiwa na alama moja kwenye kundi hilo.
Katika mchezo huo ambao Taifa Stars ilikuwa nyumbani, kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Algeria kwenda mapumziko ikiongoza kwa bao 1-0 lililofungwa na Rami Bensebaini kwa kichwa dakika ya 45.
Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote mbili kufanya mabadiliko, Algeria akitoka Adam Ounas na kuingia Mohamed Amoura huku kwa Stars akiingia Kibu Denis kuchukua nafasi ya Nickson Kibabage.
Ingizo la Kibu lilionekana kuiongezea kasi safu ya ushambuliaji ya Stars lakini hadi kufika dakika ya 54 matokeo yalibaki kuwa 0-1 na muda huo huo Novatus Dismas wa Stars alioneshwa kadi ya njano baada ya kucheza madhambi.
Dakika ya 56 Algeria kidogo wapate bao la pili baada ya Mohamed Hussein wa Stars kufanya makosa lakini nafasi hiyo haikutumiwa vyema.
Feisal Salum alipiga kiki kali iliyolenga lango la Algeria dakika ya 61 lakini likapanguliwa na kipa Adi Rais na kuwa kona.
Baada ya hapo Stars ilifanya mabadiliko kwa kuwaingiza Kelvin John na George Mpole kuchukua nafasi za Simon Msuva na Feisal Salum.
Bakari Mwamnyeto wa Stars alioneshwa kadi ya njano dakika ya 66 kwa kile kilichotafsiriwa kuushika mpira kwa makusudi.
Algeria ilifanya mabadiliko mengine dakika ya 72 kwa kuwatoa Islam Slimani na Amir Rami na kuingia Billal Brahim na Ahmed Touba.
Kipa Aishi Manula dakika ya 77 aliokoa mpira uliokuwa unaenda moja kwa moja golini baada ya kupigwa kiufundu na Bilal wa Algeria na dakika moja baadae alitoka Mohamed Belaili na kuingia Riyad Benayad kwa upande wa Algeria.
Baada ya mabadiliko hayo, Stars nayo ilimuingiza uwanjani Salum Abubakar dakika ya 80 akichukua nafasi ya Novatus Dismas.
Dakika ya 87, Algeria ilipata bao la pili kupitia kwa Mohamed Amoura aliyepiga shuti kali lililozama moja kwa moja nyavuni na mechi kumalizika kwa Stars kupoteza kwa mabao 2-0.