IMEELEZWA kuwa Rais wa Heshima ya Klabu ya Simba, Mohammed Dewji ‘Mo’ amezuia mipango ya kumleta Kocha Mkuu wa APR ya nchini Rwanda, Mohammed Adil Erradi kutokana kutokidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Erradi ni kati ya makocha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuja kuchukua nafasi ya Mhispania, Pablo Franco aliyesitishiwa mkataba wa kukinoa kikosi hicho.
Pablo alisitishiwa mkataba huo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo itoke kufungwa bao 1-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga katika mchezo wa Nusu Fainali ya Kombe la FA.
Kwa mujibu wa mmoja wa mabosi kutoka ndani ya bodi hiyo, wamepata taarifa za vigezo kutoka CAF vya makocha kutoka kwa timu shiriki katika mashindano ya Afrika ambavyo ni makocha wakuu wa klabu watatakiwa wawe na leseni ya daraja la juu ya CAF (Caf Pro Licence) au walau leseni ya CAF daraja A (CAF A licence).
Bosi huyo alisema kuwa, pia wamepata taarifa za makocha wasaidizi ni lazima wanatakiwa wawe na leseni za CAF ngazi ya daraja B (CAF B licence).
Aliongeza kuwa Mo amefuatilia kwa ukaribu vyeti vya kocha huyo na kugundua hana vigezo hivo vya CAF, hivyo haraka wameachana naye na kumtaka Mtendaji Mkuu wa timu hiyo, Barbara Gonzalez na mshauri wake, Crecentius Magori kutafuta majina matano ya makocha kati ya 100 waliowasilisha CV zao.
“Mo haraka amesitisha mpango wa kumleta Mohammed ambaye alifika hadi hapa nchini kwa ajili ya kuja kufanya mazungumzo ya kumpa mkataba wa kuja kuifundisha timu yetu.
“Maamuzi hayo yamekuja ikiwa ni siku moja imepita tangu Caf watoe vigezo vya makocha watakaotakiwa kukaa katika benchi katika michuano ya kimataifa kwenye msimu ujao.
“Kocha huyo amekosa vigezo hivyo, haraka akawataka Barbara na Magori kukutana na kuchagua makocha bora watano wenye CV nzuri ya michuano ya kimataifa Afrika kati ya hao 100 ili kumpata mmoja mwenye sifa,” alisema bosi huyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Ahmed Ally alizungumzia hilo kwa kusema kuwa: “Uongozi umeanza kuchakata CV za makocha wanaotaka kukinoa kikosi chetu na hadi hivi sasa tumezipokea zaidi ya 100.
“Na haraka tutamtangaza kocha huyo mpya mara baada ya taratibu zote kukamilika na tumepanga kumtangaza kabla ya ligi kumalizika msimu huu.”