Baada ya Simba kusikia taarifa za mshambuliaji wa ASEC Momosas, Stephan Aziz KI kumalizana na Yanga mabosi wa wekundu hao wameibuka na kutaka kumalizana naye haraka.
Simba tayari mapema walishapeleka ofa kwa mshambuliaji huyo Juni mosi wakati Yanga tayari walishaanza mazungumzo na raia huyo wa Burkina Faso.
Yanga walikutana na KI nchini Morocco jijini Berkane usiku wa Aprili 4, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya ASEC kukutana na wenyeji wao kisha wakapoteza kwa bao 1-0.
KI akifanya mazungumzo ya awali na Yanga wakifanyika chini ya makamu mwenyekiti wa kamati ya usajili ya Yanga injinia Hersi Said.
Hata hivyo jana Simba wamerudi tena kwa KI wakimpa ofa kubwa zaidi huku wakimuelezea matamu ya ndani ya klabu hiyo hatua ambayo imemtingisha mshambuliaji huyo.
KI anataka kutumia ofa hiyo mpya ya Simba kuwatingisha mabosi wa Yanga katika makubaliano aliyoyafanya juzi nchini Ivory Coast na Hersi ambaye bado yuko nchini humo.
Mshambuliaji huyo amesema Simba wameibuka wakirudi kwa nguvu wakimtumia ofa ambayo imemshtua.
“Simba wamenipigia wananiambia niachane na Yanga, lakini kuna mambo ambayo tulishafika mbali na Yanga ila nitacheza hapo Tanzania,” amesema KI