Wakati nyota wa Simba waliokuwa katika timu za taifa sambamba na wale waliokuwa na matatizo binafsi akiwamo Clatous Chama wakiinogesha kambi ya mazoezi ya timu hiyo, mabosi wa Wekundu hao wa Msimbazi wameitana ghafla jijini Dar es Salaam.
Chama alikuwa Zambia kujiuguza na kufanya kumbukumbu ya mwaka mmoja wa kifo cha mkewe, Mercy Chama aliyefariki dunia Mei, mwaka jana, na alitua nchini juzi jioni sambamba na Bwalya aliyekuwa akiitumikia timu ya taifa ya kwao na jana wote waliibukia mazoezini.
Simba inajifua kwa ajili ya mechi yao ijayo ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mbeya City, lakini siku ya mechi hiyo ya wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo watakutana kujadili mambo mbalimbali ikiwamo ishu ya kocha mpya wa kuchukua nafsi ya Pablo Franco aliyetimuliwa hivi karibuni, usajili na mipango ya msimu ujao.
Pablo alifungishwa virago kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo na mchakato wa kumpata mrithi wake unasimamiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez ambaye katika kikao hicho cha Alhamisi ijayo ataweka hadharani majina matatu ya mwisho ya walioomba kazi.
Awali, mezani kwa Barbara inaelezwa kulikuwa na majina 100 bila ya kuwepo mzawa yeyote wa Tanzania, kisha yakachujwa na kubakia 10 na sasa anamalizia kupata majina ya mwisho kabla ya kwenda kwenye kikao hicho na vigogo wenzake ili kufanya uamuzi wa pamoja.
Chanzo chetu cha habari kinasema kuwa, mchakato huo aliachiwa Barbara aufanye na mtendaji huyo amejitahidi kwa kiwango cha juu kuwasaili makocha wote kupitia simu, akiwamo aliyekuwa kocha wa Kaizer Chiefs, Stuart Batxer anayepewa nafasi kubwa na mwisho kupata majina matatu ya mwisho ambayo ni siri yake kwa sasa.
“Tunasubiri hayo majina tuyaone, tufanye uteuzi sahihi, lakini siku hiyo mbali na jambo la kocha tutajadili mambo mengine mengi yahusuyo klabu yetu ikiwemo namna tulivyokwama kutetea mataji yetu,” kilidokeza chanzo hicho kilichoomba kuhifadhiwa jina lake.
“Suala la usajili ni nani aletwe, nani aondoke (litafanyika) kwa kushirikiana na kocha anayekuja, naamini tutafanya uamuzi sahihi kwa maslahi ya wana Simba.”
Barbara alisema mchakato huo umefanyika kwa ufanisi mkubwa na kusisitiza kuwa baada ya mchujo wa majina 10 watatu pekee ndio ataenda kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi wa Simba ili kumpata zaidi ya wote atakayeweza kuivusha timu hiyo kutoka mahali ilipo sasa.