IMEFICHUKA kuwa, uongozi wa Klabu ya Azam upo katika mazungumzo na aliyewahi kuwa Beki na Nahodha wa Yanga, Lamine Moro kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ulinzi msimu ujao wa 2022/23.
Beki huyo kwa sasa ni mchezaji huru baada ya mkataba wake na Newroz SC ya nchini Iraq aliyojiunga nayo Januari mwaka huu kumalizika.
Ikumbukwe kuwa, raia huyo wa Ghana alicheza kwa mafanikio makubwa ndani ya Yanga kwa kipindi cha misimu miwili, yaani 2019/20 na 2020/21.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa mtu wa karibu na mchezaji huyo, kimesema, kuwa, tayari Azam wameanza mazungumzo na mlinzi huyo ili kuimarisha kikosi chao.
Taarifa hizo ziliendelea kubainisha kwamba, wakati mazungumzo ya beki huyo na Azam yakiendelea, Singida Big Stars na Mbeya City nazo zimeonesha nia ya kumuhitaji.
“Ni kweli mabosi wa Azam wamekuwa na mazungumzo ya muda mrefu sasa kuhitaji huduma ya Lamine Moro, bila shaka ni kwa sababu alionesha uwezo mzuri akiwa na Yanga katika kipindi anacheza Tanzania. Kama mambo yataenda vizuri basi mtamshuhudia akiwa na Azam msimu ujao.
“Lakini ukiachana na Azam, zipo klabu mbili zinamuhitaji ambazo ni Singida Big Stars na Mbeya City.”
Akizungumzia mikakati ya usajili wa kikosi chao, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Azam, Zakaria Thabith, hivi karibuni aliliambia Spoti Xtra kuwa: “Muda wa usajili bado, kwa sasa tunapambana kushinda michezo iliyosalia katika Ligi Kuu Bara.”