Na Masau Bwire.
Leo nimeona ni vizuri nitumie nafasi hii kuipongeza Yanga kwa kufanikiwa kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara baada ya kuukosa kwa misimu minne mfululizo. Hongereni sana Wananchi msimu huu mlijiandaa na kujipanga vizuri. Mlikuwa bora na imara kila eneo na idara uwanjani, lakini pia mlijiimarisha kikamilifu nje ya uwanja.
Mlistahili kuwa mabingwa pokeeni pongezi na hongera za dhati kutoka kwangu ‘Mzee wa kupapasa’.
Yanga imekuwa bora na kinara kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu mara nyingi zaidi kuliko klabu nyingine yoyote iliyowahi kushiriki ligi hiyo. Yanga imechukua ubingwa wa Bara mara 28 sasa na kumuacha kwa mbali mtani wake, Simba SC ambaye amekitwaa mara 22.
Klabu nyingine zilizofanikiwa kuwa mabingwa wa Bara na mwaka kwenye mabano ni Cosmopolitan FC ya Dar es Salaam (1967), Mseto FC ya Morogoro (1975), Pan Africa ya Dar es Salaam (1982), Tukuyu Stars ya Mbeya (1987), Coastal Union ya Tanga (1988), Mtibwa Sugar ya Morogoro (1999, 2000) na Azam FC (2013).
‘Wananchi’ wamekuwa kwenye majonzi, manyanyaso, machungu na masikitiko ya kuukosa ubingwa tangu msimu wa 2017/2018 miaka minne mfululizo ambapo kipindi chote hicho ‘Mnyama’, Simba SC, mtani wake wa jadi amekuwa bingwa mfululizo.
Yanga wana kila sababu ya kushangilia kwa kila aina ya staili inayofaa, kwani furaha waliyoipata ni kubwa baada ya kuikosa kwa miaka minne.
Ubingwa wa Yanga msimu huu umekuwa wa historia kubwa. Wamekuwa mabingwa kabla ya ligi kumalizika, lakini kubwa zaidi wakiibuka mabingwa bila kupoteza mchezo hata mmoja. Katika michezo 27 waliyoicheza wamevuna alama 67 ambazo haziwezi kufikiwa na klabu nyingine yoyote zilizowawezesha kuwa mabingwa, ikiwa imesalia michezo mitatu ligi kumalizika. Yanga imeshinda michezo 21 na kutoka sare sita tu.
Hakuna hata mmoja iliyofungwa, hiyo inathibitisha ubora na uwezo wake msimu huu kwamba ulikuwa wa viwango vya juu kuliko klabu nyingine yoyote iliyoshiriki ligi. Michezo sita iliyotoa sare ni pamoja na miwili dhidi ya Simba iliyochezwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, 11 Desemba 2021 na 30 April 2022 yote ikamalizika kwa sare ya bila mabao.
Mingine ni dhidi ya Namungo FC (1-1) Uwanja wa Ilulu – Lindi uliochezwa Novemba 20, 2021 na Mbeya City 0-0 Uwanja wa Sokoine – Mbeya uliochezwa 5 Februari 2022, Michezo mingine iliyotoa sare ni dhidi ya Tanzania Prisons (0-0) Uwanja wa Sokoine – Mbeya uliochezwa Mei 9, 2022 na mchezo ambao ulikuwa mgumu kwao ni dhidi ya Ruvu Shooting FC ‘Barcelona ya Bongo’ (0-0) Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma uliochezwa Mei 4, 2022 Wananchi aliokolewa tu na ‘mkono wa Bwana’ bila hivyo ilikuwa waelekee kibra mapema tu.
Mbali na pongezi kwa uongozi wa Yanga ukiongozwa na mwenyekiti Dk Mshindo Msola wengine wanaostahili pongezi kubwa kwa mafanikio makubwa ya klabu hiyo msimu huu ni mwekezaji Gharib Said Mohamed (GSM). Mwekezaji huyo, GSM hakuwa mbinafsi wala bahiri katika kuihudumia timu. Alishirikisha watu na alitumia fedha nyingi katika kuijenga klabu na kuifanya iwe imara na bora.
Alimtumia kijana wake, Mhandisi Hersi Said aliyeshirikiana na viongozi wengine wa klabu akiwemo mtendaji mkuu Senzo Mazingisa kuhakikisha klabu inakuwa imara na bora katika idara zote ndani na nje ya uwanja. Mwekezaji Gharib alitumia mabilioni ya fedha kuisuka Yanga na kuiweka kwenye ubora kwa kusajili wachezaji bora na wenye uwezo. Pia aliajiri na kulisuka benchi la ufundi lililosheheni wasomi wenye uwezo na weledi katika majukumu.
Ili kuhakikisha kwamba kila mmoja kwa eneo lake anawajibika ipasavyo pamoja na usimamizi mzuri uliotokana na muundo bora wa uongozi ndani ya klabu, Gharib alitoa mishahara minono kwa wachezaji na waajiriwa wengine na hakuwa na longolongo. Aliwalipa kwa wakati. Niwasihi tu kwa moyo wa upendo. Niwape ushauri wa bure Yanga ushauri wa kujenga na kuiweka klabu yenu kwenye ubora zaidi.
Endeleeni kumkumbatia GSM. Ni mtu wa watu huyo. Hana makuu. Mkono wake umenyooka na ni mrefu. Hana mkono wa birika. Namjua. Mkimtumia vizuri klabu yenu itakuwa tishio Tanzania na Afrika.
Pongezi nyingine kubwa na za pekee sana ni kwa wachezaji wote wa Yanga waliipambania timu kwa moyo wa dhati. Walijitoa, walitumia nguvu na maarifa. Walipigana. Jasho jingi liliwatoka kuhakikisha klabu inafanikiwa. Kweli wamefanikiwa mapema tu ni mabingwa wa nchi. Hongereni sana mabingwa.
Mchezaji Fiston Mayele nimpe tu kongole ya pekee na ya aina yake. Amekuwa bora msimu huu. Hakuna asiyelijua hilo. Hata watoto wadogo wanatambua kuwa mwamba wa kutetema ni bora na wanatetema naye. Labda uwe tu na roho mbaya ya kiibilisi utapinga na kuhoji ubora wake katika msimu huu.
Mayele mpaka sasa ni kinara wa kupachika mabao kwa timu yake na ligi kwa ujumla akiwa amefunga 16 akifuatiwa kwa karibu na George Mpole wa Geita Gold mwenye mabao 15. Yanga mpaka sasa imefunga mabao 45 na kufungwa saba. Wachezaji wengine wa Yanga waliofanikiwa kufunga mabao na idadi ya mabao waliyoyafunga kwenye mabano ni pamoja na Saido Ntibanzonkiza (5), Feisal Salum (5), Jesus Moloko (3), Dickson Ambundo (3) na Djuma Shabani (3). Wengine ambao mpaka sasa wamefanikiwa kufunga ni Khalid Aucho (2), Zawadi Mauya (1), Heritier Makambo (1) na Chico Ushindi (1). Wachezaji waliotoa asisti na idadi kwenye mabano ni Djuma (5), Saido (4), Feisal (4), Mayele (4), Jesus Moloko (4), na Aucho (3).
Wengine ni Farid Musa (2), Chico Ushindi (2), Kibwana Shomari (1), Yanick Bangala (1) na Abubakar Salum (1). Aidha, benchi la ufundi lililoongozwa na Nasserdinne Nabi linahitaji pongezi kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya. Limekuwa benchi bora msimu huu. Pamoja na Nabi wengine walioliunda ni Cedric Kaze, Helmi Gueldich, Razak Siwa, Hafidh Saleh, Shecky Mngazija, Mohammed Yussuf Ammar, Mahmoud Omar, Jacob Onyango, Mohammed Ali, Sadiki Mohammed, Mussa Mahundi na Athuman Muganda.
Hongereni sana wanachama, mashabiki na wadau wote wa Yanga kwani umoja, ushirikiano na mshikamano wenu katika kuisapoti timu kumewezesha ubingwa kupatikana. Jambo kubwa na la msingi kwa sasa baada ya kutangaza ubingwa wa Ligi Kuu ni kujiandaa kikamilifu kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Huko mkafanye vizuri na huko itakuwa aibu na haitakuwa na maana tena itapunguza raha na furaha ya ubingwa mkitolewa hatua ya mwanzo tu ya mashindano hayo ya Afrika.