Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta pichani na wachezaji wengine, akiwa kwenye mazoezi na klabu yake ya Fenerbahce ya nchini Uturuki ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya msimu mpya wa 2022/23.
Samatta amerejea Fenerbahce baada ya mkataba wake wa mkopo ndani ya Klabu ya Royal Antwerp ya Ubelgiji kumalizika.
Mbwana Samatta alisajiliwa na Fenerbahce akitokea Aston Villa ya Uingereza alipodumu huko kwa msimu mmoja katika mkataba wa miaka minne, ambapo walimnunua kutoka RC Genk ya Ubeligiji ambao nao walimnunua kutoka TP Mazembe ambayo alidumu nayo kwa mkataba wa misimu mitano akitokea Simba SC ya Tanzania.
Safari hiyo ya Samatta ilianzia katika klabu ya Africa Lyon zamani ikifahamika kama Mbagala Market, ambapo alicheza hapo kabla ya Simba kumsajili kwa mkataba wa miaka miwili,ambapo alitumika msimu mmoja, kisha akasusa kwa kile kilichodaiwa kutotimiziwa mahitaji ya kimkataba ikiwemo kupewa gari.
Aliendelea kukipiga Simba mara baada ya kumaliziwa mahitaji yake ya kimkataba, ambapo katika msimu wake wa pili, katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa afrika dhidi ya TP Mazembe alionyesha kiwango kikubwa kilichowavutia Mazembe waliokuwa mabingwa wa Afrika wakati huo na kuamua kumsajili kwa dau lililovunja rekodi ya usajili kwa mchezaji mtanzania.
Akiwa na TP Mazembe, Samatta alifanikiwa kushinda medali ya Klabu Bingwa Afrika, pamoja na kutangazwa kuwa mchezaji bora wa Afrika kwa wachezaji wa ligi za ndani.