UONGOZI wa Yanga, umeahidi kutorudia makosa katika michuano ya kimataifa kwa kujipanga vema kuhakikisha wanakamilisha usajili wa wachezaji wapya na kupata vibali mapema vitakavyowaruhusu kucheza michuano hiyo.
Yanga tayari imejihakikishia kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao baada ya kufanikiwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Msimu uliopita, Yanga iliwakosa baadhi ya wachezaji wa kimataifa kutokana na kuchelewa kupata Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC) akiwemo Khalid Aucho.
Msemaji wa Yanga Haji Manara, alisema msimu uliopita timu yao ilishindwa kufanya vizuri baada ya wachezaji wao tegemeo kuchelewa kupata ITC.
Manara alisema kuwa tayari wamejifunza katika hilo, hiyo ndio sababu ya kukamilisha usajili wao wa wachezaji wapya mapema ili kuhakikisha wote wanakuwepo katika kikosi chao.
Aliongeza kuwa, tayari wamekamilisha usajili wa baadhi ya wachezaji akiwemo mshambuliaji wa Kaizer Chiefs, Mzambia, Lazarous Kambole ambaye tayari ametambulishwa katika timu hiyo.
“Malengo yetu ya msimu ujao, ni kuhakikisha tunafika katika hatua nzuri kimataifa ikiwezekana kuwapita wenzetu (Simba) ambao wanaishia hatua ya robo fainali.
“Tunataka kuona msimu ujao tunacheza nusu fainali au fainali ya michuano ya kimataifa na hilo linawezekana kwetu kutokana na usajili mkubwa tulioufanya.
“Hivyo hatutaki kurudia makosa tuliyoyafanya msimu uliopita ya kuwakosa baadhi ya wachezaji wetu muhimu na tegemeo katika kikosi chetu kutokana na kukosa ITC, tumepanga kukamilisha vibali vya wachezaji wetu,” alisema Manara.