Nyota wa Kimataifa wa Tanzania, Frank Ngailo ambaye anaichezea Izimiry BBSK ya Uturuki ameingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwani tuzo ya mchezaji bora wa msimu wa Ligi Kuu ya soka la walemavu nchini humo.
Nyota huyo wa timu ya taifa ya soka la walemavu ‘Tembo Warriors’, alipata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa nchini Uturuku siku chache tu baada ya kutangazwa kuwa ni mchezaji wa bora wa mashindano ya Bara la Afrika katika soka la watu wenye ulemavu (CANAF) yaliofanyika hapa nchini.
Ngailo alikuwa na mchango mkubwa Tembo Warriors baada ya kuipeleka Kombe la Dunia ambapo aliifungia mabao matano.
Nyota huyo mzaliwa wa Ludewa mkoani Njombe tangu ajiunge wa Izmary amekuwa na mchango mkubwa licha ya kuwa aliingia katika mwa msimu ambapo hadi Ligi inamalizika Ngailo alishaifungia timu hiyo mabao tisa na kutoa assisti sita kwenye michezo 14.
Akizungumza baada ya kurejea hapa nchini kwaajili ya kujiunga na timu ya taifa anasema kuwa bado anayosafari ndefu ya kukua kisoka na amesema mchezo huu nguzo yake kubwa ni nidhamu na kujituma uwanjani.
“Bado kuna mengi nahitaji kujifunza na kuyaelewa ili nikuze kipaji pamoja na kiwango changu, soka la nje limenionyesha njia ya mafanikio katika soka hili hivyo kila siku lazima nihakikishe nimeweka kitu kipya kichwani”. anasema na kuendelea;
“Nashukuru nimeanza nyema, kocha ananikubali pamoja na wachezaji wenzangu hii imekuwa ikinipa hamasi kwakua nipo kwenye mazingira mazuri ya kuonyesha ubora wangu”. anasema Ngailo