Home Habari za michezo HUU HAPA UKWELI WOTE KWA NINI KYOMBO ALITAMBULISHWA SINGIDA BIG STARS WAKATI...

HUU HAPA UKWELI WOTE KWA NINI KYOMBO ALITAMBULISHWA SINGIDA BIG STARS WAKATI ALISHASAINI MKATABA NA SIMBA…


Juzi Jumanne Juni 21, mshambuliaji wa Mbeya Kwanza, Habibu Haji Kyombo alikuwa mchezaji wa kwanza kutambulishwa na Singida Big Stars waliopanda daraja msimu huu.

Kyombo yupo kwa mkopo wa miezi sita kwenye kikosi cha Mbeya Kwanza akitokea TS Sporting aliyokuwa nayo kwa mkopo baada ya kutokea Mamemol Sundowns ya Afrika Kusini.

Jumatatu tulielezwa ukweli wote wa Kyombo kusaini mkataba wa miaka miwili na Simba ingawa ilikuwa taarifa yenye usiri mkubwa ndani yake.

Baada ya Singida kutoa taarifa hiyo chanzo cha habari kilizungumza tena na viongozi wa juu Mbeya Kwanza na Singida huku kila mmoja akikubali kweli Kyombo alisaini Simba.

Kiongozi wa juu na mwenye maamuzi ndani ya Singida amesema hatukuwa na nia ya kumtambulisha Kyombo leo wala mchezaji yoyote yule hadi hapo msimu utakapo malizika.

“Tumeamua kumtambulisha Kyombo kutokana na kupata taarifa za uhakika kuwa Simba imemsainisha mchezaji huyo mkataba wa miaka miwili ili hali huku nyuma akiwa amechukua cha kwetu tayari,” amesema Kiongozi huyo na kuongeza;

“Kama Simba itakuwa tayari kutupatia kiasi cha Sh35 milioni ambacho tulimpatia Kyombo tunaweza kukaa nao meza moja kwa ustaarabu na tukawaachia mchezaji aende kucheza kwao,”

“Jambo kama hili limewahi kutukuta Singida wakati wa nyuma kwa Feisal Salum tulimsajili ila mwisho wa siku tulikubaliana na Yanga walitupatia gharama zetu na akaenda kucheza kwao na yupo huko hadi sasa.”

“Ila tumefanya utambulisho wa Kyombo leo baada ya kufahamu Simba imemsaini tayari mkataba wa miaka miwili wakati hapo awali alianza kusaini kwetu Singida nahisi kuna watu walimshauri vibaya, ila kwetu tulimpatia pesa hiyo na alishatumia kwenda kufanya mambo yake.”

Kiongozi wa juu wa Mbeya Kwanza, amesema Kyombo alisaini DTB kwanza kimya kimya ila Simba walikuja kumpata baadae na alishindwa kusema lolote akaenda kusaini na huko akawa amesaini timu mbili.

Amesema Kiongozi huyo Singida na Simba kote Kyombo amesaini miaka miwili na inavyoonekana uongozi wa Singida umekasirika ila mchezaji anaweza akaruhusiwa kucheza Simba lakini gharama alizochukua Singida zinatakiwa kurudishwa.

SOMA NA HII  TAKWIMU HIZI ZINASEMA DABI YA KARIAKOO ILICHEZWA KWA DAKIKA 50 TU

“Singida imeamua kumtambulisha Kyombo makusudi kwa kuwa Simba tayari taarifa zao zilishaanza kutoka kwahiyo uongozi wa Singida ulihisi unaweza kupoteza haki yao ya msingi”. alisema kiongozi huyo na kuongeza

“Na wamefanya hivyo uongozi wa Singida umeshaanza kuwabana Simba warudishe gharama ili wamchukue Kyombo kwa sababu alianza kusaini kwao na Simba wakitoa gharama hizo itaachiwa imchukue mchezaji na waendelee nae”.

“Ila Kyombo itakuwa amesaini kote kote Singida na Simba nilikuwa nataka uhakika tu wa kufahamu atakwenda kucheza timu gani kutokana na jambo hilo alilofanya”.

Kwa nyakati tofauti  Kyombo na uongozi wake ulitafutwa ili kulizungumzia sakata hilo ila simu zao hazikupokelewa.