Home Habari za michezo JINSI MSUVA ALIVYOPISHANA NA MEDALI YA UBINGWA WA KLABU BINGWA AFRIKA KWA...

JINSI MSUVA ALIVYOPISHANA NA MEDALI YA UBINGWA WA KLABU BINGWA AFRIKA KWA MISIMAMO YAKE DHIDI YA WAARABU…


SIKU moja Dijmi Traore ambaye aliwahi kutamba akiwa na klabu za Liverpool, Monaco na Marseille alimpiga dongo ‘mtania’ Mswiden, Zlatan Ibrahimovic kwa kusema yeye hana wafuasi milioni 40 kwenye akaunti yake ya Instagram na hana sanamu popote lakini ameshinda Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Zlatan ni miongoni mwa wachezaji wenye majina makubwa ambao wamepata nafasi ya kuzichezea klabu nyingi kubwa barani Ulaya kama vile, Ajax, Juventus, Inter Milan, Barcelona, ​​AC Milan, Paris Saint. Germain na Manchester United. Amecheza mara 124 kwenye michuano hiyo mikubwa na kufunga mabao 49 lakini taji hilo ameishia kulisikia tu, kama ambavyo imekuwa kwa mshambuliaji wa Kitanzania, Simon Msuva.

Huenda Msuva angetwaa ubingwa wake wa kwanza wa Afrika akiwa na Wydad Casablanca kama asingefanya maamuzi ya kurejea nyumbani. Mwanzoni mwa msimu huu wa 2021/22, uvumilivu ulimshinda mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Tanzania na kuamua kurudi zake Bongo na kusikilizia baada ya miamba hiyo ya Morocco kushindwa kutimiza kwa wakati makubaliano yao ya kimkataba.

Wakati aliporejea zake Tanzania, Msuva aligoma kuongelea kiundani hicho ambacho kilitokea zaidi alieleza kwa ufupi kuwa ni changamoto ya kimaslahi ambayo amekumbana nayo, “Hili suala lipo sehemu husika (FIFA) tusubiri tuone maamuzi ambayo yatatolewa,” alikaririwa akisema.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga aliondoka Wydada Casablanca akiwa ameifungia mabao mawili kwenye michezo miwili aliyoichezea kabla ya hatua ya makundi ambayo wababe hao waliitambuka kwa kishindo na kutinga robo fainali, nusu na kuitandika Al Ahly kwenye mchezo wa fainali kwa mabao 2-0.

Katika mahojiano maalumu ambayo kocha wa Wydad, Walid Regragui alifanyiwa ameeleza vile ambavyo mambo yalivyokuwa huku akilitaja jina la Msuva na mastaa wengine kwenye klabu hiyo mara bada ya kuondoka na jinsi walivyopambana na kuwa wafalme wa Afrika.

“Hakuna aliyefikiria tungekuwa hapa mwanzoni mwa mwaka. Tulimpoteza Ayoub El Kaabi, ambaye ni mfungaji bora wa pili [yeye ni wa tatu] Uturuki. Mohamed Ounajem, Walid El Karti na Simon Msuva wote waliondoka mwanzoni, ilitubidi tujiaminishe kuwa hakuna ambalo linashindikana na lazima maisha yaendelee.”

SOMA NA HII  VIGOGO SIMBA WADINDISHIANA KUHUSU NANI WA KUACHWA KATI YA MUGALU NA BOCCO...KAGERE HANA MTETEZI...

“Ningependa sana kuwashukuru mashabiki, walinisaidia sana,” alisema Regragui.

Wakati akijiunga na Wydada Casablanca akitokea Difaa El Jadida, katika moja ya mahojiano ambayo alifanya na safu hii, Msuva aliamini kuwa anaweza kutwaa ubingwa wa Afrika akiwa na miamba hiyo.

“Wydad ni miongoni mwa klabu kubwa, kwangu ni hatua naamini kuwa Mungu atanifungulia milango zaidi na nitatimiza ndoto yangu ya kutwaa ubingwa wa Afrika,” alisema Msuva.

Kisa cha Msuva kupishana na ndoo ya Ligi ya Mabingwa Afrika kimepishana kidogo na kile cha Zlatan ambaye mwaka 2010 alikaribia kutwaa ubingwa huo kwa Ulaya lakini maamuzi ya kuamua kuondoka Inter Milan na kujiunga na Barcelona yalimfanya kuona marafiki zake wakibeba taji hilo.

Barcelona ikiwa na Zlatan ilifungashiwa virago vyao kwenye hatua ya nusu fainali kwa kutandikwa jumla ya mabao 3-2 na Inter Milan , huenda kama angesalia basi angebeba msimu huo kwani chama lake hilo la zamani lililokuwa linanolewa na Jose Mourinho lilitwaa ndoo hiyo kwa kuitandika Bayern Munich kwenye mchezo wa fainali iliyochezwa Santiago Bernabeu, Madrid kwa mabao 2-0.