Home Habari za michezo KIGOGO TFF AFUNGUKA ALIVYOHAMA NYUMBA KISA MORRISON KUJIUNGA NA SIMBA…”HANS POPE ALIKUWA...

KIGOGO TFF AFUNGUKA ALIVYOHAMA NYUMBA KISA MORRISON KUJIUNGA NA SIMBA…”HANS POPE ALIKUWA MKALI MUDA WOTE”…

 


UMEPITA mwaka mmoja na ushei tangu sakata la Bernard Morrison alipokuwa Yanga kutua Simba baada ya kuwazidi akili mabosi wa Yanga kwenye kesi iliyofunguliwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kabla ya kesi kuhamia CAS na kutolewa hukumu mwaka jana.

Licha ya muda mrefu kupita tangu sakata hilo kumalizika, lakini mtu aliyebebeshwa mzigo wa kuhukumu kesi hiyo ndani ya TFF kupitia Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, imebaki kumbukumbu isiyofutikwa kichwani mwa aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Elias Mwanjala.

Mwanjala amefanya mahojiano maalumu na kufunguka mambo mengi juu ya kesi hiyo na namna ilivyoweza kumlaza nje ya nyumba yake kwa siku kadhaa ili kuitatua baada ya nyota huyo kusaini Simba huku Yanga wakidai bado ni mchezaji wao kwa madai kwamba alikuwa amesaini mkataba mpya.

Anabainisha kesi hiyo ilikuwa na vitu vingi, huku vingine vilikuwa nje ya uwezo wake, lakini alijitahidi kuhakikisha anafanya uamuzi kwa kufuata haki licha ya kuwa ni Yanga lialia.

Anakiri huenda kesi hiyo ndiyo iliyomfanya akapigwa rungu la kufungiwa miaka miwili kujihusisha na soka kwa kuwa Uchaguzi wa TFF ulikuwa Septemba, huku yeye akifungiwa Desemba akihoji kwa nini baada ya kesi ya Morrison afungiwe wakati uchaguzi ulishafanyika. Ebu endelea naye…!

SAKATA LA MORRISON

Mwanjala anasema aliwahi kupitia kesi mbalimbali akiwa ndani ya kamati hiyo, lakini kesi ya Morrison baada ya kusajiliwa Simba ilikuwa ngumu na ilimfanya kupata maadui kutoka Yanga timu anayoipenda katika maisha yake.

“Ile kesi ilikuwa kubwa sana na ilitawala hisia za watu wengi hasa wananchi wa pande zote mbili ambao walikuwa wakisubiri kwa hamu nje ya TFF kujua uamuzi wa kamati, na mimi nilijulikana naipenda Yanga aisee nilipata simu nyingi kutoka kila kona sehemu nyingine siwezi kuzitaja,” anasema.

“Nawashukuru sana viongozi wa TFF hasa Rais Wallace Karia katika ile kesi wala hakuwa na sauti yoyote. Nakumbuka aliniambia mwenyekiti nakuachia wewe, ndio maana nimekuamini na kukupata hiyo kamati, simama kwenye sheria mwenye haki iende kwake.

SOMA NA HII  RAGE AIBUKIA YANGA....AMWAGA SIFA KAMA ZOTE..."WANACHOKIFANYA HUWEZI KUKIONA POPOTE PALE:...

“Halikuwa shauri dogo lile na ndio maana hata sisi tuliamua kufungiana wenyewe, nakumbuka nilimtoa nje Hayati Zacharia Hanspope alikuwa anakuwa mkali tu bila sababu, nikamtimua kwenye kikao akakataa, nikamshtaki kwa Karia akaniambia nawaachia wenyewe mfanye uamuzi, siwezi kumsifia Karia ila penye sifa mpeni.”

Mwanjala anasema na kubainisha kwamba uamuzi wa kamati yake uliwaudhi na kuwafurahisha watu na hakukuwa na jinsi.

BM3 AMHAMISHA NYUMBA

Kiongozi huyo anasema kesi ile ilikuwa ngumu kwani ilisababisha hata kubadilisha magari kila siku kutokana na hisia za wengi akiamua kujilinda ili kuimaliza salama, huku akimtanguliza Mungu kumuongoza.

“Baada ya matokeo ya sakata hilo imewafanya hadi Yanga wenzangu wanichukie na kuonekana adui kwao, lakini ile kesi ilikuwa ngumu na baada ya kesi niliondoka zangu kwenda kwetu Kyela. Baada ya siku moja kulala hotelini niliona isiwe tabu niondoke zangu na uzuri watu wengi walikuwa hawapajui kwangu,” anasema Mwanjala.

“Nashukuru sana Mungu kesi ilipoenda CAS majibu yalikuja na kunipa heshima mimi na kamati yangu, sitaki kuiongelea sana kesi hiyo kwani naweza kuleta vurugu nyingine. Lakini likae vichwani mwa watu kesi ilikuwa na presha ila nilisimamia misingi, haki na taratibu.” Mwanjala anawataka viongozi wa kamati hiyo kuacha mahaba na kufanya kazi kwa haki.

Anasema sakata hilo lilimfanya akae nje ya Dar es Salaam mwezi mzima ili kupisha upepo wa kesi hiyo ambayo ilizua gumzo nchi nzima na hata alipokuwa kwao akitokea mgeni ambaye hakumuelewa, aliamua kujificha.

Credit:- MWANASPOTI