Home Habari za michezo KUHUSU UFUNGAJI BORA MSIMU HUU…MPOLE NA MAYELE WATEGEANA…KILA MMOJA AKIMBILIA NJIA YAKE…

KUHUSU UFUNGAJI BORA MSIMU HUU…MPOLE NA MAYELE WATEGEANA…KILA MMOJA AKIMBILIA NJIA YAKE…


VINARA wa kucheka na nyavu Ligi Kuu Bara, Fiston Mayele wa Yanga na George Mpole wa Geita Gold FC, ni kama wameanza kuwekeana mitego kwa kila mmoja kuzuga kama hawazii kutwaa Kiatu cha Dhahabu kwa kuibuka mfungaji bora wa ligi hiyo mwishoni mwa msimu.

Mayele na Mpole kila mmoja ana mabao 16 wakati huu Yanga ikiwa imebakiza mechi tatu na Geita Gold michezo miwili kabla ya msimu wa Ligi Kuu 2021/22 kumalizika hapo Juni 29, mwaka huu.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wetu, kila mmoja ameweka wazi kuwa lengo lake ni kuipa timu matokeo na si kuwazia kumaliza kinara wa ufungaji katika ligi hiyo.

Mayele alimwambia mwandishi wetu juzi kuwa kwa upande wake anahitaji kutafuta matokeo kwa ajili ya kusaidia timu yake na hataki presha ya kuwaza anashindanishwa na nani katika mbio za kuwania tuzo ya ufungaji bora.

“Tulitaka ubingwa, hilo tumefanikiwa na sasa hivi hakuna tunachokitafuta ni kumaliza ligi bila kufungwa nahitaji kusaidia timu yangu kupata matokeo na si ushindani na Mpole kuwa mfungaji bora,” alisema Mayele.

Wakati Mayele akieleza hayo, Mpole alisema lengo ni kufunga magoli katika michezo yao iliyobakia ili washike nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo.

“Lengo ni kushika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hii japokuwa ina ushindani mkubwa,” alisema Mpole.

Mpole alisema anawashukuru mashabiki kwa ushirikiano wanaoendelea kuwaonyesha katika kipindi hiki cha Ligi Kuu ya NBC.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUBWAGWA NA SIMBA...OKWA AAMUA KUANIKA YOTEE...AMTAJA ALIYEMFELISHA..