Home Habari za michezo RASMI…KUELEKEA MSIMU UJAO WA LIGI YA MABINGWA AFRIKA…CAF WAIPA SIMBA HADHI SAWA...

RASMI…KUELEKEA MSIMU UJAO WA LIGI YA MABINGWA AFRIKA…CAF WAIPA SIMBA HADHI SAWA NA AL AHLY YA MISRI…


WAKATI Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), likitangaza msimu wake wa michuano Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika utaanza rasmi Agosti 12, mwaka huu, wawakilishi wa Tanzania wenye historia nzuri katika mashindano hayo, Klabu ya Simba itakuwa miongoni mwa klabu 10-bora zitakazoanzia raundi ya kwanza.

Kwa upande wa Tanzania, tayari wawakilishi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika wamejulikana, ambao ni mabingwa wapya wa Ligi Kuu Bara, Yanga pamoja na Simba iliyojihakikishia kumaliza nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo.

Ikumbukwe msimu ujao wa michuano ya CAF, Tanzania itawakilishwa na timu nne, mbili Ligi ya Mabingwa na idadi kama hiyo Kombe la Shirikisho Afrika, ambapo hadi sasa mchuano ni mkali kwenye Ligi Kuu timu zikiwania kumaliza nafasi nne za juu.

Hata hivyo, kama Yanga iliyotinga Fainali ya Kombe la FA, itafanikiwa kutwaa taji hilo dhidi ya Coastal Union, hiyo inamaana timu zitakazoshika nafasi ya tatu na ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu, ndizo zitakazoiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika, lakini Coastal ikilitwaa, itaungana na mshindi wa tatu wa Ligi Kuu kushiriki kinyang’anyiro hicho cha kimataifa.

Kwa mujibu wa Kanuni za CAF, klabu zinazoshika nafasi 10-bora kwenye viwango vya Shirikisho hilo, kama zitafuzu kushiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa kulingana na kanuni za mashirikisho ya nchi zao, ndizo ambazo huanzia raundi ya kwanza (First Round) na ambazo zipo nje ya 10-bora huanzia raundi ya awali (Preliminary Round).

Hata hivyo, Simba licha ya kushika nafasi ya 14-bora kwenye viwango vya klabu vya CAF, imeangukia kuanzia raundi ya kwanza baada ya Klabu ya RS Berkane iliyokuwa nafasi ya tano kwa ubora, Pyramids (9), Étoile du Sahel (10) na Orlando Pirates (11), kushindwa kufuzu michuano hiyo kupitia ligi za nchi zao.

Katika viwango vya Klabu vya CAF vilivyotolewa wiki iliyopita, namba moja inashikiliwa na Al Ahly ikifuatiwa na Wydad Casablanca, Espérance de Tunis, Raja Casablanca, RS Berkane, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe, Zamalek, Pyramids, Étoile du Sahel, Orlando Pirates, Horoya FC, Petro de Luanda na Simba ikishika nafasi ya 14.

SOMA NA HII  TSHABALALA,KAPOMBE HALITETE WASAIDIWE

Kwa maana hiyo, kushindwa kufuzu michuano hiyo kwa Klabu za RS Berkane, Pyramids, Étoile du Sahel na Orlando Pirates, moja kwa moja zinatoa nafasi kwa Horoya FC iliyokuwa nafasi ya 12, Petro de Luanda (13) na Simba nafasi ya 14, kupanda na kuingia ndani ya klabu kumi bora zitakazoanzia michuano hiyo raundi ya kwanza.

Hivyo, Simba, Horoya FC na Petro de Luanda zitaungana na Al Ahly, Wydad Casablanca, Espérance de Tunis, Raja Casablanca, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe pamoja na Zamalek kuwa klabu 10 zitakazoanzia raundi ya kwanza kwenye michuano hiyo inayoongoza kwa utajiri barani Afrika kwa ngazi ya klabu.

Nafasi ya Simba kuingia hatua hiyo imetokana hasa na Étoile du Sahel kupoteza mchezo wao wa mwisho dhidi ya Monastir kwa kuchapwa mabao 2-0 ugenini juzi, hivyo kukosa nafasi ya kuongoza kundi lao kwenye Ligi Kuu Tunisia, na kutoa nafasi kwa Club Africain kuongoza kundi na kufuzu Ligi ya Mabingwa, ambapo sasa itakuwa miongoni mwa zikazoanzia raundi ya awali.

Wawakilishi wengine wa Tanzania kwenye Ligi ya Mabingwa, Yanga ambao wametwaa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu, pamoja na klabu zingine zilizofuzu Ligi ya Mabingwa ambazo hazipo kwenye 10-bora, wao wataanzia raundi ya awali na kama wakipata matokeo ya jumla nyumbani na ugenini, wataingia kwenye droo ya kupangiwa moja kati ya klabu 10-bora hizo, kucheza tena mechi ya nyumbani na ugenini ili kusaka nafasi ya kufuzu hatua ya makundi.