Home Habari za michezo LIGI KUU MSIMU UJAO KUENDA KWA MFUMO WA KIULAYA ULAYA…TAREHE YA KUANZA...

LIGI KUU MSIMU UJAO KUENDA KWA MFUMO WA KIULAYA ULAYA…TAREHE YA KUANZA YATAJWA…KIPYENGA KULIA AGOSTI 17…


Ligi Kuu Bara msimu ujao 2022/23 itaanza Agosti 17 mwaka huu na kumalizika Mei 27 mwakani huku Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Almasi Kasongo akitoa sababu ya ligi ya msimu huu kuchelewa kumalizika.

Kasongo amewahakikishia wadau wa soka kuwa ligi ya msimu ujao haitakuwa na mambo mengi na itamalizika kwa wakati.

Kasongo alisema Ligi Kuu Bara itaanza Agosti 17 na kumalizika Mei 27 mwakani wakati ligi ya Championship ( Daraja la Kwanza) itaanza Septemba 17 na kumalizika Mei 13 mwakani huku First League ( daraja la pili) ikitarajiwa kuanza Oktoba 15 na kumalizika Aprili Mosi mwakani.

“Kuna mambo mawili yaliyosababisha tukachelewa kumaliza ligi , kwanza ikumbukwe msimu wa 2020/2021 kulikuwa na janga la corona lililosababisha ligi kusimama na kuchelewa kumalizika.

“Hali hiyo ilipelekea ligi ya msimu huu kuchelewa kuanza na hivyo kuchelewa kumalizika pia licha ya kwamba tulijitahidi kutokuwa na mechi za viporo, ” amesema Kasongo na kuongeza;

” Changamoto nyingine inayosababisha kubadili badili ratiba ni kalenda ya Shirikisho la Soka Afrika ( CAF) kutoka wakati sisi tukiwa tumeshatoa kalenda zetu na mipango yetu.

” FIFA huwa wanatoa kalenda yao mapema lakini Caf ilikuwa changamoto kwani wakati sisi tunatangaza kalenda zetu wao wanakuwa bado , badae wakitoa ndio inapelekea na sisi kubadili ratiba wakati ligi inaendelea.

Kasongo alisema msimu ujao hakutakuwa na mabadiliko ya ghafla ya ratiba kwani wametoa kalenda kulingana na kalenda ya CAF na FIFA.

“Safari hii CAF wametoa kalenda zao zote mapema ikiwemo ya mashindano ya CHAN, Afcon, na mashindano ya klabu ndio maana hata kalenda tuliyoitangaza imeweza kuakisi kalenda yao.

” Msimu huu tumerudi kwenye kanuni yetu ya kuanza ligi Agosti na kumaliza Mei mwaka unaofuata na matarajio yetu msimu ujao tutaenda vizuri ,” amesema Kasongo.

Pia Kasongo alisema ligi kuu msimu ujao itaendelea kama kawaida hata wakati wa Fainali za kombe la Dunia zitakazoanza Novemba mwaka huu.

“Ligi ya msimu ujao haiwezi kusimama kwa ajili ya mashindano ya kombe la Dunia kwa sababu katika klabu zetu hakuna wachezaji wengi ambao mataifa yao yanashiriki fainali hizo ukiondoa Mali ambayo baadhi ya wachezaji wapo hapa nchini, ” amesema Kasongo.

SOMA NA HII  SIKU CHACHE BAADA YA KUPIGWA CHINI KUTENGENEZA JEZI ZA SIMBA...VUNJA BEI AIBUKA NA KUANIKA HAYA...