Home Habari za michezo KUELEKEA FAINAL YA KOMBE SHIRIKISHO KESHO KUTWA….MAYELE ANAJAMBO LAKE CAF….

KUELEKEA FAINAL YA KOMBE SHIRIKISHO KESHO KUTWA….MAYELE ANAJAMBO LAKE CAF….

Habari za Yanga

Wakati kikosi cha Yanga kikirejea salama nchini kikitokea Afrika Kusini, mshambuliaji nyota wa timu hiyo, Fiston Mayele, amesema ndoto yake sasa ni kuona wanatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu.

Yanga imetinga fainali za mashindano hayo baada ya kuiondoa Marumo Gallants ya Afrika Kusini wakati USM Alger ya Algeria wao wameitoa ASEC Mimosas kutoka Ivory Coast.

Mayele, alisema inawezekana Yanga kutwaa ubingwa wa michuano hiyo ya kimataifa kutokana na wachezaji wa timu hiyo kuwa na viwango vikubwa.

Mayele alisema amejiandaa kuendeleza ushindani katika mchezo wa fainali ya dhidi ya USM Alger utakaochezwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Nilishasema tangu Lubumbashi (DRC), katika mechi dhidi ya TP Mazembe hatuwezi kuishia robo fainali, leo (sasa), tuko fainali, tumefanikiwa kwa sababu kikosi chetu kina wachezaji wakubwa, nyinyi wenyewe mmeona, tunavyocheza kwenye Ligi Kuu na michuano hii ni tofauti, tuko kwenye fainali ni furaha na shangwe. Kwenye ligi ya ndani nimeshaonyesha vitu vingi.

Sasa nilitaka kuonyesha katika michuano ya kimataifa, mchezaji mkubwa unatakiwa kufanya vyema katika mechi kubwa pia. Mimi nataka kupambania timu yangu ili tuchukue kombe, ingawa USM Alger ni timu nzuri kwa sababu pia imefika fainali, kikubwa ni kufanya vyema katika mechi ya kwanza,” alisema Mayele.

Aliongeza amefurahi timu yake kukata tiketi ya kucheza fainali katika mashindano hayo msimu huu na anaamini wataendelea kufanya vyema kwenye mchezo wao unaofuata.

Mshambuliaji huyo alisema amepanga kuonyesha kiwango kikubwa ili kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa michuano hiyo kwa mara ya kwanza.

“Tunashukuru tumefanikiwa kuingia kwenye hatua ya fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuiondoa Marumo Gallants katika hatua ya nusu fainali, sasa tunahitaji kuendeleza ushindi kwenye mechi inayofuata,” Mayele alisema.

Nyota huyo alisema mara baada ya kufunga goli katika mechi ya marudiano, alifarijika na anataka kuacha historia ndani ya Yanga pamoja na kutangaza jina lake duniani kupitia mpira.

“Katika Ligi Kuu Tanzania Bara nimefanya kazi kubwa sana kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, malengo yangu ni kuiendeleza kasi hiyo kimataifa, ninaamini tunaweza,” alisema.

Mkongomani huyo aliongeza anafahamu mchezo wao wa kwanza wa fainali utakuwa mgumu na wenye ushindani lakini kwa pamoja wachezaji wamejipanga kupambana ili kuhakikisha wanapata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.

“Nitaipambania timu yangu nikiwa na malengo ya kuisaidia kupata ushindi tukiwa hapa nyumbani pamoja na kwenye mchezo wa marudiano ambao tutaucheza ugenini, tunawaomba Watanzania waendelee kutuombea ili tufanye vizuri katika hatua hii ya fainali,” Mkongomani huyo alisema.

Aliweka wazi pia amefurahi kusikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, ameongeza dau la zawadi hali inayowaongezea morali ya kupambana.

“Siri ya mafanikio yangu inatokana na nidhamu niliyokuwa nayo ikiwamo kufuata vyema maelekezo ninayopewa na benchi lake la ufundi. Ninawashukuru Watanzania kwa ushirikiano wanaoendelea kutuonyesha katika michezo yetu yote,” aliongeza mshambuliaji huyo.

SOMA NA HII  DIARA AZIDI KUIPAISHA JUU LIGI YA TANZANIA...AITWA TENA MALI KWA KOMBE LA DUNIA...