Home Habari za michezo MANARA:- ” HATA NIKIPEWA UKUU WA WILAYA NITAKATAA….KUNA WATU WANACHUKI NA MIMI…”

MANARA:- ” HATA NIKIPEWA UKUU WA WILAYA NITAKATAA….KUNA WATU WANACHUKI NA MIMI…”

Habari za Yanga

Aliyekuwa Ofisa Mhamasishaji wa Klabu ya Yanga, Haji Sunday Manara amesema kuwa hahitaji cheo chochote cha Serikali kwenye nchi ya Tanzania na hata kama akiteuliwa na mamlaka atakataa kwani yeye lengo lake kubwa lilikuwa ni kulisemea soka la Tanzania lakini ameonewa na kudhulumiwa haki yake, hivyo atatangaza kuachana kabisa na masuala ya soka.

Manara amaesema hayo ikiwa ni takribani mwaka mmoja tangu alipofungiwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kujihusisha na masuala ya soka ndani nan je ya nchi kwa kipindi cha miaka miwili na faini ya Tsh milioni 10 kwa kosa la kuwadhalilisha viongozi wa TFF akiwemo Rais wa shirikisho hilo, Wallace Karia wakati wa mechi ya Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam msimu wa 2021/22 ambapo Yanga iliibuka bingwa kwa mikwaju ya penati baada ya sare ya bao 3-3 katika dakika 90.

“Mimi soka liko kwenye damu, sio mtu wa kuja, nimezaliwa kwenye familia ya soka kuanzia babu zangu upande wa mama, baba zangu na mimi mwenyewe. Nimecheza mpira, nimefundisha mpira na nimeusemea mpira kwa manufaa makubwa tu lakini ninaona watu wanachukizwa na ukubwa wa jina langu wanatamani hata waniue au wanivunje nitembee na mguu mmoja, ndiyo raha yao.

“Wanadhani pengine ninahitaji vyeo vyao, sina mpango wa kuwa Rais wa Shirikisho, kuwa Mkuu wa Wilaya (DC), kuwa Mkuu wa Mkoa (RC) wala kuwa Waziri ama madaraka yoyote kwenye nchi hii na hata kama nikiteuliwa nitakataa, sina ndoto hizo, ninahitaji kuwa Haji Bugatti. Sina uwezo wa kwenda kuhimiza kilimo na mifugo mimi uwezo wangu na ndoto yangu ilikuwa ni kuisemea football ambayo nimeiishi kwa miaka mingi.

“Nimedhulumiwa haki yangu wakati sikufanya kosa lolote kwa sababu tu ya roho mbaya za watu wachache ambao wamekuja kwenye soka kutafuta maslahi yao wenyewe. Mimi sikuja kwenye soka kutafuta maslahi, nimezaliwa kwenye soka kwa nini nipoteze uhai wangu au familia yangu kwa mambo kama haya? Hivi karibuni nitatangaza kuachana kabisa na soka ndani ya siku 10 mpaka 14 zijazo.

“Hata baadhi ya viongozi waliopo kwenye mpira sasa hivi walidhulumiwa haki zao tukapigana na mwisho wa siku wakapata haki zao lakini hao ha oleo hii wanashiriki kunidhulumu haki yangu na Serikali ipo kimya, kwa nini niendelee na mambo ya mpira? Soka sio baba yangu wala mama yangu, nitaachana nalo.

“Siwezi hata kuzungumzia kundi la Afcon ambalo Taifa Stars imepangwa, kwa nini nizungumzie Tanzania ambayo mimi hainitaki? Nizungumzie kundi linanihusu nini mimi? Hao TFF si ndio wananifanyia majungu kila siku? Mimi sihusiki na mpira, wapangwe na nani shauri yao mimi hainihusu.

“Mimi kwanza sio Mtanzania kwanza, kama ningekuwa Mtanzania nchi yangu isingekubali mimi nidhulumiwe. Sidhani kama nina haki hata kwenye nchi hii kwa sababu ningekuwa na haki, raia ninadhulumiwa na watu wako kimya, sasa naizungumzia nini? Nilishaizungumzia sana, nimeshaitangaza sana, nimekewenda sana AFCON kwa pesa zangu na sijawahi kukosa, nani anajali? Watu wanajali vyeo vyao na maisha yao,” amesema Haji Manara.

SOMA NA HII  BAADA YA KICHAPO CHA ZANACO...YANGA WAJIPOOZA LEO..WAICHAPA TIMU YA DARAJA LA KWANZA GOLI ZA KUTOSHA