Home Habari za michezo RASMI…MBEYA KWANZA YAWA YA KWANZA KUSHUKA LIGI KUU MSIMU HUU…GEITA GOLD WAISOGELEA...

RASMI…MBEYA KWANZA YAWA YA KWANZA KUSHUKA LIGI KUU MSIMU HUU…GEITA GOLD WAISOGELEA CAF KININJA…


Matokeo ya kupoteza mchezo wao mabao 2-1  Mbeya Kwanza  dhidi ya Ruvu Shooting imewafanya kushuka daraja na msimu ujao kucheza tena Ligi ya Championship.

Timu hiyo ambayo ilipanda msimu uliopita, ilihitaji ushindi  ili kuendelea na matumaini ya kubaki Ligi Kuu lakini mambo yamekuwa magumu kwao.

Katika mchezo  uliopigwa uwanja wa Majimaji mjini Songea, wenyeji hawakuonesha soka la ushindani sana na kuwapa nafasi wapinzani kutakata na kujihakikishia kubaki Ligi Kuu kwa pointi 31 wakibaki na mechi moja.

Mabao ya Ruvu Shooting yalifungwa na Full Maganga na Rashid Juma na kuifanya Mbeya Kwanza kubaki na alama zao 24 na mchezo mmoja dhidi ya Simba utakaopigwa Juni 29 mjini Songea.

Mbeya Kwanza hata kama watashinda mechi yao ya mwisho, watafikisha alama 27, ambazo hazitatosha kuwashusha Biashara United walioshinda leo 1-0 dhidi ya KMC na kufikisha pointi 28, huku ikisubiri mwenzake hususani Tanzania Prisons ambao nao hali si hali.

Prisons kwa sasa wako nafasi ya 15 kwa pointi 26, ambapo kesho Jumapili watawakaribisha Simba ikiomba dua ya alama tatu ili kujiweka pazuri kabla ya kumaliza msimu dhidi ya Ruvu Shooting huko mkoani Pwani, Juni 29.

Wakati huohuo, Geita Gold imejihakikishia pia nafasi nne za juu baada ya kuikandika Polisi Tanzania 1-0 na kukusanya alama 45 huku ikitanguliza mguu mmoja kimataifa ikisubiri matokeo ya mchezo wa fainali ya kombe la shirikisho (ASFC) kati ya Coastal Union dhidi ya Yanga, Julai 2 jijini Arusha.

SOMA NA HII  YANGA JIANDAENI..PABLO AANZA NA MAMBO MATATU SIMBA..MORRISON NDANI...CHAMPION LEO..