Home Uncategorized YANGA YATOA MSIMAMO KWA CARLINHOS

YANGA YATOA MSIMAMO KWA CARLINHOS


LICHA ya kutoonekana uwanjani kwa wiki kadhaa, Yanga wametoa msimamo wao kuhusiana na mustakabali wa staa Muangola, Carlos Carlinhos.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Yanga, Hersi Said aliiambia gazeti la Mwanaspoti jana kwamba hawana mpango wa kumtema staa huyo kwani wana malengo naye ya muda mrefu.

Alisema kuwa mchezaji huyo alikuwa nje akiuguza majeraha na daktari amewahakikishia atakaa sawa.

“Carlinhos ameumia na alikuwa majeruhi ni muda sasa akiuguza nyonga yake. Kuna muda ambao alipewa pumzika huku akipata matibabu na sasa ameanza mazoezi taratibu kwa maelekezo ya madaktari.

“Klabu tunafuatilia kila kitu na tumeambiwa anaweza kuwa tayari labda kuanzia Januari, sote tunasubiri na sio kweli kwamba tunataka kumtema huyu bado ni mchezaji wetu mpaka mkataba wake wa miaka miwili utakapomalizika,” alisema Hersi ambaye Mwanaspoti linajua kabla ya Januari kumalizika atamshusha nchini straika Mkongomani, Idriss Mbombo wa Nkana FC.

Mashabiki wa Yanga kwenye mitandao ya kijamii wameonyesha kumisi mishuti ya mchezaji huyo mahiri kwenye friikiki, kona na mipira ya kurusha.

Yanga ipo kambini jijini Mbeya na kesho Alhamisi watafunga mwaka kwa kucheza mkoani Rukwa na Prisons kwenye mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.

Katika mechi hiyo mbali na kumkosa Carlinhos, hata Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na kipa kijana Ramadhan Kabwili na mshambuliaji Yacouba Songne nao wana walakini kutokana na afya zao kutetereka.

Hersi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Uwekezaji wa GSM ambao ni miongoni mwa wadhamini wa Yanga alidai wameshtukia hali ya kukamiwa vibaya kwa Saido ambapo wamewataka waamuzi kuwa makini katika kumlinda mchezaji huyo ili aweze kufanya kazi yake vyema.

Credit- Mwanaspoti

SOMA NA HII  BREAKING: SARRI AFUNGASHIWA VIRAGO JUVENTUS