Home Habari za michezo UKWELI MCHUNGU….SIMBA HAIJABADILIKA KWA CHOCHOTE KILE…FUKUTO LINALOVUMA CHINI KWA CHINI LITALIPUKA….

UKWELI MCHUNGU….SIMBA HAIJABADILIKA KWA CHOCHOTE KILE…FUKUTO LINALOVUMA CHINI KWA CHINI LITALIPUKA….


KUNA vitu vingine vinachekesha sana. Ni kama hii sinema inayoendelea pale Simba kwa sasa. Ni vichekesho vitupu.

Tulianza kusikia kuna fukuto ndani ya klabu ya Simba. Habari zikavuja chini kwa chini. Lakini sasa mambo yote ni hadharani. Fukuto lipo kweli, tena kubwa sana.

Nilipata mshtuko kusikia kauli za Kassim Dewji ‘KD’ mapema wiki hii. KD amesema mambo mengi ambayo kwa nafasi yake usingetarajia ayatamke hadharani. Unadhani kwanini? Subiri nitakwambia.

Kwanza, KD ni kiongozi mwenye ushawishi mkubwa sana pale Simba. Amewahi kuwa katibu mkuu. Baadaye akawa katibu wa Kamati ya Usajili ya klabu. Na kisha akawa mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi. Achilia mbali udugu wake na mwekezaji wa timu.

Ni mtu ambaye amekulia Simba kwa miaka mingi. Anafahamu mazuri na mabaya. Anafahamu vyema namna ya kuzungumza. Pia sio mtu wa kuzungumza sana mambo ya ndani ya klabu kwenye vyombo vya habari. Lakini wiki hii ametoka hadharani na kusema.

Kassim amedai kuwa wapo waajiriwa wengi pale Simba ambao hawana sifa. Ajabu ni kwamba pamoja na hilo, bado Bodi ya Wakurugenzi haina mamlaka ya kuwawajibisha.

Pili, Kassim amedai kuwa mtendaji mkuu wa klabu hiyo ni kama yupo juu ya bodi. Kwa kifupi ni kwamba mtendaji mkuu anaweza kuamua mambo kivyake bila kuishirikisha nodi. Ni ajabu na kweli.

Hii ndio Simba mpya tuliyoambiwa. Simba iliyobadilika. Aah wapi! Simba bado ni ileile.

Unawezaje kujinasibu kuwa timu imekwenda kwenye mchakato wa mabadiliko kama bado inaajiri watu wasio na sifa? Unawezaje kusema hadharani kuwa Simba inaendeshwa kisasa kama mtendaji mkuu ana uamuzi mkubwa kuliko bodi?

Kumbuka kwamba Bodi ya Wakurugenzi ya Simba inaundwa na pande mbili. Ina wawakilishi wa mwekezaji na upande wa wanachama. Je mtendaji Mkuu anamwakilisha nani?

Kila mtu anafahamu alipotoka mtendaji mkuu. Alikuwa akifanya kazi kwenye ofisi ya mwekezaji. Pengine ndiko anakotoa ujasiri anaodaiwa kuwa nao na KD. Pengine ndicho kinachomfanya aone kuwa yupo juu ya bodi.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUONDOSHWA LIGI YA MABINGWA.....MORRISON AZUA JAMBO MSIMBAZI...

Vipi nguvu ya upande wa wanachama iko wapi? Hakuna. Ni kama tu sehemu kivuli. Sehemu pekee ambayo upande wa wanachama unaweza kuwa na kauli ni ndani ya Bodi ya Wakurugenzi. Lakini tumeshaambiwa kuwa hawana nguvu juu ya mtendaji mkuu. Inafikirisha sana.

Ukichimba ndani zaidi pale Simba utaambiwa namna mambo hayaendi. Kila kitu kinategemea huruma ya mwekezaji. Hakuna mfumo mzuri wa uendeshaji, timu inategemea zaidi mtu.

Siku mwekezaji akifurahi mnapata mishahara kwa wakati. Siku akinuna mtasubiri sana.

Mfumo wa posho bado ni kizungumkuti. Bado hakuna utaratibu mzuri wa nini wachezaji wanapata wakishinda mechi na fedha hizo zinatoka wapi. Timu inategemea zaidi fedha za mfukoni mwa watu.

Ni kweli mwekezaji anatoa zaidi fedha zake binafsi kuendesha timu. Lakini huo ndio uwekezaji wenyewe.

Mwekezaji anatakiwa kufahamu kuwa anapotoa fedha sio kwamba anaombwa au anafanya hisani, bali ndio biashara aliyoamua kufanya na Simba. Ni jukumu lake kutoa fedha. Anatakiwa kutoa tena na tena.

Lakini pamoja na kwamba mwekezaji amemwachia Salim Abdallah ‘Try Again’ nafasi ya kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, bado ana uamuzi mwingi binafsi. Pengine hana imani na usimamizi wa Try Again. Kama hana imani kwanini alimteua?

Nimekuwa kwenye soka la Bongo kwa miaka mingi. Miaka zaidi ya 20 sasa. Namfahamu vizuri Salim Abdallah. Ni mtu makini sana katika kazi zake. Anaimudu vizuri Simba, lakini kwanini sasa itokee tu mtendaji mkuu anakuwa na nguvu zaidi yake ndani ya klabu kama tulivyomsikia KD? Nadhani ni mfumo mbovu uliowekwa na mwekezaji. Pengine mchakato wa mabadiliko ya Simba kuna mahali ulikwama. Wanapaswa kurudi nyuma na kujitazama upya ili waende sawa.

Credit:- MwanaSpoti