IMEFAHAMIKA kuwa wachezaji wa Yanga wanatarajiwa kupewa Sh 700Mil kutoka kwa mdhamini wao GSM kama bonasi baada ya juzi kubeba Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC).
Yanga wamefanikiwa kubeba kombe hilo juzi kwa kuwafunga Coastal Union kwa penalti mabao 4-1 baada ya timu hizo kutoka sare ya kufungana 3-3 mchezo uliopigwa juzi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
Timu hiyo, imeweka rekodi kubwa katika msimu huu ya kucheza mashindano yote waliyoshiriki bila ya kufungwa ikiwa chini ya Kocha Mkuu, Mtunisia, Nasreddine Nabi.
Taarifa zinasema kuwa wachezaji hao muda wowote watakabidhiwa mamilioni hayo na Rais wa Makampuni wa GSM, Ghalib Said Mohammed ambaye alikuwepo uwanjani katika mchezo huo wa fainali.
Mtoa taarifa huyo alisema bonasi hiyo watapewa kama sehemu ya ahadi aliyowapa wachezaji hao katikati ya msimu huu ambao tayari Yanga wamebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Aliongeza kuwa bonasi hiyo inafikia Sh 700Mil kutokana na ubingwa wa Ligi Kuu Bara Sh 200Mil, Nusu Fainali ya FA kwa kuwafunga Simba 200Mil, Kombe la FA 200Mil na nyingine ni kutokufungwa (Unbeaten) Sh 100Mil.