KABLA ya usajili haujakamilika Simba itatikisa anga kwa kushusha mashine mbili za maana ambazo ni funga kazi. Mmoja ni beki na mwingine ni straika.
Mpaka jana Simba ilikuwa imemtambulisha Moses Phiri Pamoja na Habib Kyombo pekee lakini wameshakamilisha mazungumzo na straika wa Rivers United, Mnigeria Nelson Esor Okwa (28) na jana walipanga kumtumia mkataba pamoja na kumalizana na klabu yake ili dili hilo limalizike haraka iwezekanavyo.
Siyo huyo tu, Kocha Zoran Maki amewaambia viongozi kwamba; “Kuna beki mmoja nilikuwa naye Waydad Casablanca namtaka, nafasi yake isizibwe.” Simba ambayo inakamilisha mipango ya kwenda kambini nchini Misri Julai 15 mwaka huu, iko kwenye harakati za kumalizana na mastaa hao wawili kwa haraka na wanaamini kwamba huo utakuwa usajili wao mtamu zaidi katika dirisha hili.
Awali, Simba ilikuwa inataka beki wa kati kutokea Ethiopia lakini kocha ameangalia faili, hakulielewa, akawaambia viongozi waachane naye wamchukue huyo wa kwake ambaye bado jina limekuwa siri kubwa.
Inaelezwa mabosi wa Simba wamefanya mazungumzo na Okwa ila aliwaeleza alikuwa na mkataba wa miaka mitatu na Rivers na umebaki mwaka mmoja kwa maana hiyo kabla ya kufanya lolote wanatakiwa kumaliza hilo na Simba wanaelekea kukamilisha.
Mabosi wa Simba walifanya mazungumzo na uongozi wa Rivers na wamekubaliana kununua mkataba wa mwaka mmoja uliobaki wa Okwa kisha mchezaji kutaja maslahi binafsi anayohitaji, ambayo nayo wameafikiana.
Kinachosubiriwa wakati huu ni Simba kuingiza pesa kwenye akaunti ya Rivers pamoja na mchezaji ili kupewa barua, pamoja na kumpa mkataba wa miaka miwili waliyokubaliana.
Muda wowote kuanzia leo Simba itamtumia mkataba Okwa na kusaini kama itakuwa tayari imekamilisha mambo hayo. Okwa ni nahodha wa kikosi cha Rivers na amekiongoza kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu ya Nigeria msimu huu. Simba wamevutiwa naye baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye mechi mbili dhidi ya Yanga katika Ligi ya mabingwa msimu uliopita.
Alipotafutwa Okwa alisema amefikia hatua nzuri na Simba ambacho anasubiri ni utaratibu wa usajili wake kukamilika.
“Mazungumzo yetu yamekwenda vizuri na tumekamilisha kila kitu, ambacho tunasubiri wakati huu ni Simba kufuata huo utaratibu kisha nisaini mkataba wao kama watautuma nikiwa huku Nigeria au nitakuja kukamilisha kila kitu hapo Tanzania,” alisema Okwa aliyezaliwa Desemba 26, 1993 na kuongeza;
“Kama hakutakuwa na mabadiliko na kila kitu kikienda tulivyokubaliana nitakuja Simba na msimu ujao nitakuwa mchezaji wa kikosi hicho, tusubiri muda utaongea.
“Simba ni timu kubwa hapa Afrika, ikitokea nafasi ya kuhitajika, mchezaji yoyote kama ilivyo kwa upande wangu si rahisi kupoteza fursa kubwa kama hiyo.”
Mwenyekiti wa bodi Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ alisema msimu huu watakuwa na kikosi bora zaidi,