Home Habari za michezo WAKATI PAZIA LA LIGI KUU LIKIFUNGWA NA TUZO JUZI..NBC BANK WAIBUKA NA...

WAKATI PAZIA LA LIGI KUU LIKIFUNGWA NA TUZO JUZI..NBC BANK WAIBUKA NA TAMKO HILI JIPYA…AJIRA 3,000 ZATAJWA..


Benki ya NBC imetaja mafanikio saba makubwa yaliyotokana na uamuzi wake wa kudhamini ligi kuu ya soka Tanzania bara ‘NBC Premiere League’ ikiwamo kuimarika kwa mnyororo wa uchumi, ajira pamoja na kuimarika kwa mazingira ya wachezaji na vilabu.

Mwezi Oktoba mwaka jana (2021) Benki hiyo ilichukua uamuzi mzito wa kudhamini ligi kuu Tanzania Bara kwa mkataba wa miaka mitatu ambapo wadau walikuwa na maoni mbalimbali juu ya uamuzi huo.

Akizungumza wakati wa hafla ya utoaji tuzo kwa wachezaji na vilabu vilivyoshiriki ligi kuu msimu wa 2021/2022, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC Theobald Sabi alisema uamuzi huo umezaa matunda makubwa kwa benki, tasnia ya michezo pamoja na taifa kwa ujumla.

“Mchango ambao udhamini huu umeleta kwa taifa letu unatupa sisi Benki ya NBC, kama Benki ya kizalendo inayomilikiwa kwa kiasi kikubwa na Serikali yetu, wasaa wa kusimama kifua mbele, na kujivunia kuweza Kufungua fursa za maisha kwa watanzania wenzetu na kusaidia kupambana na umasikini,” alisema Sabi.

Alitaja manufaa hayo ikiwa kuimarika kwa biashara na mnyororo wa uchumi ambapo alieleza kuwa timu 16 zilizoshiriki kwenye Ligi Kuu ya NBC zimesaidia kuboresha biashara katika miji yao na hivyo kukuza vipato vya familia kupitia mauzo ya bidhaa na huduma mbalimbali.

Kuhusu ajira alisema ligi ya NBC imesaidia kutoa ajira 3,000 za moja kwa moja kwa wachezaji, waamuzi, wauguzi, walimu na wanahabari wa michezo.

Aidha, alisema ligi hiyo imesaidia katika kuongeza makusanyo ya kodi kwa Serikali kupitia mauzo ya tiketi, kodi za ongezeko la thamani na kupitia mishahara ya wachezaji na viongozi.

“Benki ya NBC pia inajivunia kutumia jukwaa hili katika kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujumuishaji wananchi katika sekta rasmi ya fedha. Kupitia mechi za ligi hii, tumefanikiwa kufungua akaunti mpya, kutoa elimu ya fedha na mikopo ya uwezeshaji kwa maelfu ya wananchi,” alisema Sabi.

Eneo jingine ni kuwezesha upatikanaji wa bima kwa wachezaji na viongozi ambapo imesaidia kuongeza hamasa na uhakika wa ajira zao.

SOMA NA HII  KUELEKEA PAMBANO LAKE NA 'MZUNGU'....MWAKINYO APEWA ONYO...MSIRI WAKE WAKARIBU AFUNGUKA MENGI MAPYA...

Pia, alitaja eneo la kuibua vipaji ambapo alisema ligi hiyo imekuwa na mchango mkubwa katika kuibua vipaji akiwataja wachezaji kama Reliants Lusajo wa Namungo FC na Abdul Sopu wa Coastal Union ambao wameng’ara kupitia ligi hiyo.

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa alisema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuboresha mazingira ya soka nchini.

“Hili ni jambo la kujivunia na ni matumaini yetu kuwa tutapiga hatua kubwa kisoka duniani” alisema.

Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia alisema ligi kuu ya mwaka huu imekuwa bora zaidi kutokana na maandalizi mazuri na udhamini mzuri huku akiwapongeza washindi.

“TFF inawapongeza washindi wote kwenye ligi kuu na kombe la shirikisho na waliopanda kushiriki Ligi kuu nasi tutatoa ushirikiano kwa timu zote zitakazoshiriki,” alisema.