Kama ulikuwa unadhani Abdallah Shaibu ‘Ninja’ ataondoka Yanga, basi pole yako, kwani beki huyo wa kati bado yupo sana Jangwani baada ya mabosi wa timu hiyo kumuongezea mkataba.
Ninja ambaye alirejeshwa Yanga msimu uliopita kutoka Marekani, amesainishwa mkataba wa mwaka mmoja ili kupata nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wake, baada ya msimu ulioisha kushindwa kucheza kutokana na kusumbuliwa na majeraha.
Awali uongozi wa timu hiyo, ulipanga kumuongezea mkataba Ninja bila kumpa dau la usajili, lakini imekuwa tofauti wamempa na kumboreshea mshahara wake.
Habari za ndani kutoka kwa mmoja wa viongozi wa timu hiyo, zilisema Ninja alipewa mkataba huo kutokana na mchango wake wa nyuma na baada ya msimu uliosha kusumbuliwa na majeraha wakaona wampe nafasi nyingine.
“Yanga imeona umuhimu wake na ndio maana ilimtibia na kumpa nafasi nyingine ya kuitumikia klabu yake ni kati ya wachezaji wenye uzalendo na timu,” alisema na kuongeza;
“Isingekuwa kusumbuliwa na majeraha ni kati ya wazawa ambao wangefanya kazi nzuri sana msimu huu.”
Chanzo hicho kiliendelea kusema tayari Ninja amepona majeraha yake, hivyo huduma yake inatarajiwa kutumika kwenye timu msimu ujao.
Wakati Ninja akibakishwa wenzake kama Yassin Mustafa, Deus Kaseke, Paul Godfrey ‘Boxer’, Chico Ushindi, Heritier Makambo na Erick Johola wanatajwa kutemwa.