HABARI kubwa kwa sasa nchini Tanzania ni usajili wa wachezaji kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.
Klabu zilizotia fora kwa usajili mpaka sasa ni tatu, ambazo ni Simba, Yanga na Azam FC, zote za jijini Dar es Salaam.
Kila klabu imeshusha vifaa, wachezaji wa kimataifa ambao inaamini watakuwa chachu kuelekea msimu ujao kwani zote zitaiwakilisha Tanzania katika michuano ya kimataifa. Simba na Yanga zitacheza Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Azam itaenda kuchuana katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Azam imewasajili wachezaji raia wa Ivory Coast, Tape Edinho, Kipre Junior, Mnigeria Issa Ndala, kipa Ali Ahmada ambaye ni raia wa Comoro na Mghana James Akamanko.
Lakini kama ilivyo kwa soka la Tanzania, macho ya mashabiki yapo kwa klabu za Simba na Yanga.
Kwa upande wa Simba, yenyewe inaendelea kusajili, na tayari imeshaanza kutangaza baadhi ya wachezaji iliyowatia mikononi.
Usajili wao uliotikisa mpaka sasa ni wa mchezaji wa kimataifa wa Ghana, Augutine Okrah.
Ni usajili uliotikisa nchini pamoja na kwao Ghana, wakifuatilia mchezaji huyo ambaye kwa maoni ya wengi alifaa kwenda kucheza soka la kulipwa barani Ulaya.
Ndiyo mchezaji pekee kama si wawili wanaoitwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa wakicheza soka la kulipwa Afrika.
Wakati Simba wakifanya hivyo, Yanga nayo ikashusha kifaa kutoka Burkina Faso ambacho kilikuwa kinacheza soka la kulipwa nchini Ivory Coast kwenye klabu ya Asec Mimosas. Anaitwa Stephane Aziz Ki.
Nao umekuwa ni usajili wa kushtusha kwa mashabiki wa soka, hasa barani Afrika ambao sasa wameanza kuiangalia Tanzania na usajili wake kwa wachezaji wa Afrika Magharibi.
Vita au mbwembwe za usajili hapa Tanzania hazikuanza leo. Ni za enzi na enzi. Tofauti yake zamani zilikuwa zikisajili wachezaji wenye umri mkubwa au wenye viwango duni kutoka Afrika Magharibi, lakini wachezaji wa kawaida walikuwa wakisajiliwa kutoka Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda.
Baadaye tukaanza kuona Simba na Yanga zikibadilika na kuanza kusajili wachezaji wenye viwango vikubwa kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Kwa sasa tunaanza kuona zimeanza kusajili wachezaji wa viwango vya juu kutoka Afrika Magharibi.
Haya ni maendeleo makubwa katika soka la nchi hii kwa sababu Ligi Kuu Tanzania Bara itaanza kufuatiliwa mpaka kwenye nchi hizo, baada ya mashabiki wa Kenya, Rwanda, Burundi, Zambia wakifanya hivyo kwa ajili ya kuona wachezaji wao.
Lakini bado binafsi natatizwa na kitu kimoja. Nacho ni waamuzi wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Pamoja na timu hizi zinasajili wachezaji wa viwango vya juu na kuziacha klabu zingine zikipambana kunyang’anyana wachezaji wa Kibongo wenye viwango vya kawaida, lakini baadhi yao maamuzi yao yanakuwa ya kuzibeba hizo hizo timu zenye wachezaji wenye uwezo.
Huu ni unyanyasaji na ukatishaji tamaa kwa wachezaji hasa wa Kitanzania. Kwanza hawaimbwi kama hawa wa nje. Sawa ni kwa sababu ya viwango vyao. Lakini hata pale wanapopambana kutaka kuonyesha uhodari wao na kuionyesha Afrika na dunia kama wanaweza, lakini unakuta waamuzi wanawafanya waonekane hawajui.
Timu ya Ligi Kuu inaweza kucheza kimkakati na mfumo mzuri huku wachezaji wake Wazawa wakijitolea kwa asilimia 100 kupambana na Simba au Yanga zenye nyota wa kigeni, lakini kwa makusudi au bahati mbaya wamekuwa wakiwatoa kwenye mchezo kwa kuzibeba timu kubwa.
Kutokana na gharama ambazo Simba na Yanga inatumia kwenye usajili, ifike wakati waamuzi waache viwango vifanye kazi uwanjani na si kuwaongezea wachezaji wa kigeni viwango na kuwashusha kwa makusudi Watanzania waonekane hawajui.
Kama timu ina wachezaji bora iachwe ishinde kwa uwezo wake. Ni dhambi na aibu kubwa kuidhulumu timu yenye wachezaji wenye viwango vya kawaida ambao wamepambana na kutoa jasho kuwadhibiti wale wa viwango vikubwa, lakini mwamuzi analazimisha waonekane hawajui chochote kwa kuzibeba tu timu kubwa.