Kiungo mpya wa Simba, Mnigeria, Victor Akpan, ameanza kwa kuwachimba mkwara wapinzani wao Yanga kwa kuwaambia kuwa wasubirie moto wake katika mchezo wa Ngao ya Jamii ili apunguze maumivu ya kukosa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la Azam Sports (ASFC) akiwa na Coastal Union.
Kiungo huyo amejiunga na Simba kwa mkataba wa miaka miwili akitokea Coastal Union ambapo katika mchezo wake wa mwisho wa fainali ya ASFC, maarufu kama FA, alikuwa ni mmoja wa wachezaji waliocheza mchezo huo ambao Yanga walifanikiwa kuibuka na ubingwa.
Simba inatarajiwa kucheza na Yanga Agosti 13, mwaka huu kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii ikiwa ni kiashiria cha kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.
Akpan alisema kuwa moja kati ya kazi kubwa zilizopo mbele yake kwa sasa ni kuhakikisha anapambana katika mchezo ujao wa Ngao ya Jamii kuipa ushindi Simba ili kupunguza maumivu yake ya msimu uliopita.
“Najua mchezo wetu wa kwanza kimashindano msimu huu utakuwa dhidi ya Yanga katika Ngao ya Jamii lakini nataka kwangu uwe wa tofauti kwa sababu nataka kuona naanza na furaha nikiwa na timu mpya kwa kuhakikisha tunapata ushindi.
“Unajua hawezi kuwa kitu chepesi kwa sababu nitacheza mbele ya mashabiki wengi wa Tanzania na itakuwa ni mara ya kwanza kwangu lakini nitahitaji kuwa bora ili nipunguze yale maumivu ya kukosa ubingwa wa kombe la FA msimu uliopita ambao nikiwa na Coastal tulipoteza dhidi yao,” alisema Akpan.