Klabu ya Simba ipo kwenye wakati mgumu kuhakikisha inamalizana na straika wa Vipers, Cesar Manzoki ambaye mkataba wake umebaki miezi miwili, huku miamba hiyo ya Uganda ikigoma kumuachia ikidai shilingi milioni 100.
Manzoki ni miongoni mwa wachezaji ambao walitarajiwa kuungana na kikosi cha Simba kilichoweka kambi nchini Misri kujiandaa na msimu ujao wa 2022/23, lakini hadi sasa mambo yamekuwa magumu.
Kigogo mmoja kutoka ndani ya Simba, amesema kwamba: “Manzoki ni miongoni mwa wachezaji ambao tumemalizana naye na tayari alishasaini mkataba, changamoto kubwa ni kwa upande wa waajiri wake wa zamani Vipers ambao wamegoma kumuachia kutokana na kubakisha miezi miwili kwenye mkataba wake, huku wakidai fedha kubwa ambayo haiendani na muda aliobakisha hapo.
“Kwa sasa tunafanya taratibu zote kuhakikisha suala hili tunalimaliza ikiwezekana kuwasiliana na FIFA ili mchezaji huyu aungane na wenzake kambini kwani muda unazidi kwenda, sisi tulishamalizana naye kila kitu, kilichobaki ni yeye kumalizana na waajiri wake.
“Hivyo sisi kama uongozi tunaendelea na utaratibu kuona suala hili linaisha kwa wakati na kama ikishindikana FIFA watalimaliza.”