Beki wa kati Malickou Ndoye raia wa Senegal amefunga rasmi usajili wa Azam FC katika dirisha kubwa la msimu wa 2021/2022 akiwa ni nyota mpya wa tisa kusajiliwa na matajiri hao wa Chamazi.
Ndoye (22), amesaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia Azam akitokea katika klabu ya Teungueth inayoshiriki Ligi Kuu Senegal ambayo pia ni timu aliyotoka kiungo wa Simba Pape Sakho.
Nyota huyo siku chache zilizopita alikuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya Senegal kilichoshiriki michuano ya COSAFA nchini Afrika Kusini iliyotamatika Jumapili iliyopita na kuisaidia timu yake kumaliza katika nafasi ya tatu.
Usajili huo unakuwa wa mwisho kwa Azam katika dilisha kubwa hili na hapo awali iliwatambulisha mastaa watano wa kigeni na watatu wazawa.
Kipa Mcomoro Ali Ahmada, Viungo Waivory Coast, Tape Edinho na Kipre Junior, Mnigeria Isah Ndala, Mghana James Akaminko na Ndoye ndio wachezaji wapya wa kigeni waliosajiliwa na Azam kipindi hiki.
Wazawa ni beki Nathanael Chilambo kutokea Ruvu Shooting, kiungo, Cleophace Mkandala aliyekuwa Dodoma Jiji na mshambuliaji Abdul Seleman ‘Sopu’ kutoka Coastal Union.
Aidha ili kuwa bora zaidi msimu ujao, Azam iliongeza makocha watatu katika timu yao wakiweo Wahispania wawili, Dani Cadena ambaye ni kocha wa makipa na Mikel Guillen mtaalamu wa misuli na viungo sambamba na Kali Ongala atakayekuwa anawanoa washambuliaji tu.
Azam imeanza kambi rasmi jana kwenye viwanja vyake vya Azam Complex na Julai 22 itapaa kwenda nchini Misri katika mji wa El Gouna itakapokita kambi maalumu kuendelea kujifua kwajili ya mashindano ya ndani na Kombe la Shirikisho Afrika.