Kiungo wa zamani wa Yanga, Mapinduzi Balama ameelezea kupitia kipindi kigumu hasa baada ya kusumbuliwa na majeraha ya muda mrefu akiwa Yanga, huku akikiri kuwa haikuwa riziki kwake kuitumikia timu hiyo.
Mchezaji huyo amekwenda mbali zaidi na kueleza kuwa Yanga imempa funzo ambalo litakuwa ni mwongozo katika maisha yake mapya kisoka katika timu nyingine atakazokuwa.
Mchezaji huyo ambaye amekuwa nje ya uwanja msimu mzima uliopita baada ya kuvunjika kifundo cha mguu wa kushoto mwishoni mwa msimu wa 2019/20 na kufanyiwa upasuaji nchini Afrika Kusini, alisema malengo yake ndani ya Yanga hayakutimia.
“Nilihitaji muda zaidi ili kulipa kile ambacho sijakitumikia Yanga kwa kuwa majeruhi, lakini imekuwa tofauti baada ya kunipa barua ya kuachana nayo,” alisema.
“Sitakuwa miongoni mwa wachezaji wa Yanga msimu ujao baada ya mkataba wangu kumalizika. Hawajaniongezea mkataba mpya, japo ndoto zangu Yanga hazikutimia.
“Nilihitaji muda zaidi ili nipate nafasi ya kucheza na kulipa kile ambacho sijakifanya kutokana na majeraha niliyokuwa nayo.
“Nimeishi maisha mazuri ndani ya timu hiyo tangu mwanzo hadi nilipopewa mkono wa kwaheri. Sitawasahau Wanayanga kikubwa nilichokipata ndani ya timu hiyo nitakifanyia kazi nikiwa kwenye timu yangu mpya ambayo nitakwenda msimu ujao.”
Hata hivyo, amefichua kwamba bado hajajua atacheza timu gani japo ana ofa ya timu mbili, kati ya Dodoma jiji na Geita Gold ambao mazungumzo bado yanaendelea na mojawapo kati ya hizo ndipo atacheza kwa msimu ujao.