KIUNGO mkabaji wa Simba, Victor Akpan amekabidhiwa majukumu mapya baada ya kupewa jezi namba sita aliyokuwa anavaa beki wa zamani wa timu hiyo, Pascal Wawa.
Wawa anayetajwa kutua Singida Big Stars baada ya kumaliza mkataba na Simba akidumu kwa misimi mitatu alikuwa bora kwenye safu ya ulinzi ndani ya misimu hiyo kabla ya ujio wa Henock Inonga ambaye alimuondoa kikosi cha kwanza.
Akpan amepewa jezi aliyoanza kuitumia tangu ametua ardhi ya Tanzania akiitumikia Coastal Union ambayo ameifanyia makubwa na kuishawishi Simba kumwaga mamilion ili waweze kupata saini yake.
Ametua Simba na kupata bahati ya kukabidhiwa jezi hiyo ambayo alianza kuitumia kwa mara ya kwanza kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Ismaily, Mirsi uliomalizika kwa sare ya bao 1-1.
Akpan ana kazi ya ziada kuonyesha thamani yake kwani sio tu kurithi jezi ya Wawa aliyetwaa mataji mawili kwenye misimu mitatu ili aweze kuitendea haki jezi hiyo. Kiungo huyu msimu uliopita akiwa Coastal Union aliifunga Simba bao na kupoteza mchezo wa kukubali kipigo cha mabao 2-1.
Mbali na Akpan, Simba imemkabidhi kiraka wa timu hiyo, Nasoro Kapama jezi namba tano ambayo ilikuwa inavaliwa na Israel Mwenda anayesemekana kutolewa kwa mkopo.